Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema serikali kupitia Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imepiga hatua kubwa katika urasimishaji wa biashara na ulinzi wa ubunifu ndani ya kipindi cha siku 100, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi na kuwawezesha wananchi hususan vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa
wakati akizungumza waandishi wa habari na watanzania kuhusu mafanikio makubwa ya siku 100 katika sekta ya viwanda na biashara baada ya uchaguzi mkuu,
Kapinga alisema katika kipindi hicho kampuni 4,233 zimesajiliwa, ambapo kampuni 2,915 ni za vijana. Aidha, majina ya biashara 7,498 yamesajiliwa, yakihusisha majina 4,742 yanayomilikiwa na vijana.
Waziri Kapinga aliongeza kuwa alama za biashara na huduma 881 zimesajiliwa, leseni za viwanda 141 zimetolewa ambapo viwanda 129 vinamilikiwa na vijana, pamoja na utoaji wa leseni za biashara kundi A zipatazo 4,907.

Alisema mafanikio hayo yametokana na msukumo mkubwa uliowekwa na Wizara kupitia kampeni za elimu kwa umma, vipindi vya redio na televisheni, semina pamoja na maonyesho mbalimbali yaliyolenga kuwahamasisha wananchi kurasimisha biashara zao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, urasimishaji wa biashara umeleta manufaa makubwa kwa wananchi, ikiwemo vijana wengi zaidi kumiliki biashara zilizosajiliwa, hali inayowawezesha kupata mikopo, kushiriki zabuni na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi kwa kutumia majina ya biashara yaliyosajiliwa kisheria.
Aidha, alieleza kuwa kuongezeka kwa biashara rasmi kumechangia kuongeza ajira, kukuza mapato ya serikali na kuimarisha ushindani wa haki katika soko la biashara nchini.
Katika kuendeleza ajenda ya uwezeshaji wa vijana, Waziri Kapinga alisema Wizara kupitia Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha maarifa ya kibiashara na ujasiriamali.
Alieleza kuwa chuo kimepata hati ya ekari 15.64 za ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Hai, sambamba na kuwasilisha andiko la mradi wa HEET lenye thamani ya dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kupanua uwezo wa kutoa mafunzo.
Waziri huyo alisema kuwa katika mafunzo ya ujasiriamali na uatamizi wa biashara, vijana 1,240 wamepatiwa mafunzo katika kampasi za CBE Mwanza na Mbeya, huku vijana 228 wakisajiliwa katika programu za uatamizi wa biashara ambapo mafunzo haya yalifanyika mwezi Desemba 2025.

“Klabu tisa za ujasiriamali zimeanzishwa katika shule mbalimbali, ambapo vijana 215 wa shule za sekondari wamepata mafunzo ya ubunifu wa miradi midogo, uendelezaji wa mitaji na uanzishaji wa biashara ndogo,” alisema.
Waziri Kapinga aliongeza kuwa programu ya uatamizi wa biashara (Business Incubation) imeanzishwa rasmi, ambapo vijana 278 wamesajiliwa kama washiriki wa awali katika miradi ya TEHAMA na utengenezaji wa bidhaa.
Alisema hatua hizi zinaweka msingi imara wa kulijenga taifa lenye kizazi cha vijana wenye ujuzi wa kibiashara, wanaojiajiri na kuajiri wengine, hivyo kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na biashara nchini.


