VIJANA WAUNGANA NA RAIS DK.SAMIA KUSHEREKEA ‘BIRTHDAY ‘

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WAKATI Rais Dk.Samia Suluhu Hassan leo Januari 27  akisherekea kutimiza miaka 66 tangu kuzaliwa kwake,vijana wa maeneo mbalimbali waliopo jijini Dar es Salaam wamekusanyika pamoja ili  kusherekea siku hiyo kwakuelezea mambo mbalimbali anayoendelea kuyafanya kwa wananchi hasa vijana katika uongozi wake.

Akizugumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Bora Jijini Dar es Salaam Mratibu wa Taasisi ya Together For Samia, Gulatone Masiga,, amesema lengo la mkusanyiko huo ni kuwakutanisha vijana wa kizazi kipya pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kwa Taifa ili kumuonesha Rais heshima na shukrani.

Masiga ambaye ni mmoja wa waandaaji wa hafla hiyo amesema Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayefungua milango ya fursa kwa vijana, mlezi wa ndoto za kundi hilo  na anayesikiliza mawazo ya kizazi kipya huku akisimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa usawa kote nchini.

Amesema Rais Dk.Samia amefanya mambo mengi kwa ajii ya vijana ikiwemo ujenzi wa vyuo vya ufundi,ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambazo zinazalisha ajira kwakundi kubwa la vijana nchini kwa sasa.

“Hii si sherehe tu, bali ni ishara kwamba vijana wa kizazi kipya na wananchi wenye mapenzi mema kwa Taifa tunatambua uongozi unaotujali na kutupa nafasi. Tumeona ni vyema kuandaa shughuli ya kuwakutanisha ili kuonesha upendo na heshima kwa Rais ambaye ni mlezi wa vijana na maendeleo ya Taifa,” amesema Masiga.

Amesema vijana walioshiriki katika hafla hiyo ni wa kizazi kipya ambao wamenufaika kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Rais Dkt. Samia katika takribani miaka mitano ya uongozi wake.

Tumeona hatuna sababu ya kutofurahia siku ya leo na kuonesha upendo wetu kwake,” alisema, akisisitiza kuwa uongozi wa Rais umehakikisha maendeleo yanafika kila kona ya nchi.

Kwa upande wake, kijana mzalendo Dorcas Mshiu amesa anasimama kifua mbele kusherehekea siku hiyo maalumu ya Rais Dkt. Samia, akieleza kuwa Rais huyo amekuwa mama anayewakumbuka vijana na kuwafungulia fursa mbalimbali.

Amesema kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, vijana wengi wameanza kusajili biashara zao, hali inayoonesha kuwa mazingira ya biashara yamefunguka.

“Rais Dkt. Samia amefungua milango ya uwekezaji, hali iliyoongeza ajira kwa vijana wengi nchini… vijana wanaojiajiri wamenufaika na mkakati maalumu wa mikopo yenye riba ya asilimia nne, unaowawezesha kuanzisha na kuendeleza biashara zao hivyo Mama yetu asituache sisi kama GENZ; tunasema mama ni mlezi wa GENZ,” amesema Dorcas.

Katika hafla hiyo vijana waliweza kukata keki yakusherekea siku hiyo kama ishara ya upendo kwa Rais Dk.Samia.