PROFESA MKENDA AWAAGA WANAFUANZI WANAOENDA KUSOMA AFRIKA KUSINI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adoph Mkenda amewataka vijana 16 wanaoenda  masomoni nchini Afrika Kusini kupitia ufadhili wa masomo wa Samia Scolarship kusoma kwa bidii ili kuweza  kusaidia kuendelea kuleta mapinduzi ya teknolojia nchini.

Vijana hao ni kati ya 100 waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi na hisabati ya juu ambapo awamu hiyo ya kwanza wanaenda katika chuo cha Johannesburg kilichopo Afrika Kusini huku kundi jingine lililobaki likitarajiwa kupelekwa nchini Ireland

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Januari 30, 2026,Profesa Mkenda  alisema lengo lakuanzisha ufadhili huo ni kupata watalaam wabobevu wanaopelekwa katika vyuo mahili vilivyopo katika nchi mbalimbali kwa ufadhili wa serikali.

Alisema wanafunzi hao wanaenda kusoma masuala ya data sayansi akili unde na vitu vingine vinavyohusiana ambapo wanafunzi wote waliopata alama za juu katika mtihani wa Taifa  na ufaulu mzuri wa hisabati ya juu.

“Tunapeleka watoto kwenda kusoma nje baada ya kumaliza kidato cha sita,kwenye kundi hili kuna watu mbalimbali wengine watoto wafugaji na wengine hata kama familia zao zina uwezo mkubwa sana ilimradi tu wawe wameongoza na kupata alama nzuri. 

“Hawa wa kwanza wanaenda kusoma chuo kikuu cha Johannesburg Afrika ya Kusini ambacho ni chuo bora na kizuri sana moja ya sifa ya chuo hiki hasa katika maswala ya kompyuta na injinia ni vile vyuo ambavyo wanamuunganiko mkubwa sana wa taaluma ya darasani na shughuli na kazi za viwandani kila mwanafunzi atakaposoma hapa mtaona wenyewe mtakuwa mnasoma darasani na unaunganishwa kwenye makampuni ya teknolojia kupata uzoefu wa kile ambacho mnakisoma darasani,”alisema Profesa Mkenda.

Alisema wanafunzi wataoenda kusoma chuo cha Johannesburg watapata fursa za kufanya kazi kwenye makampuni ya teknolojia na kuwafanya kuja kwa bora kwakuwa  wanahakikisha kwamba mtu unafanya kile unachokifanya darasani unakiunganisha mara moja na maswala ambayo wanajifunza.

Alisema kati ya wanafunzi 50 waliofaulu vizuri sana katika tahasusi za sayansi zinazojumuisha hisabati ya juu wanatoka katika shule za aina mbalimbali wawili kati yao chimbuko lao sekondari za serikali 20 shule binafsi 30.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Nombo, amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye programu za kimkakati kama Samia Scholarship Extended DS/AI, kwa kuwa zinasaidia kujenga msingi wa maendeleo ya muda mrefu kupitia sayansi na teknolojia.

Profesa Nombo amewataka wanafunzi kuzingatia kuwa wao ni mfano kwa vijana wengine waliopo mashuleni, na kwamba nafasi hizo zinapatikana kwa misingi ya ushindani wa kitaaluma (merit-based), hivyo wanafunzi wajitahidi katika masomo hasa ya sayansi na TEHAMA.

Amesema uwepo wa taasisi kama Nelson Mandela Institute of Science and Technology umechangia kwa kiasi kikubwa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kitaaluma na maisha, ikiwemo financial management na stadi za karne ya 21.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzie waliopata ufadhili huo Malaika  Florence alisema safari yao ilikuwa ndefu sana tangu walivyoanza kidato cha tano na badae kupelekwa katika Shule ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya maandalizi ya safari.

“Tumefundishwa masuala ya financial management tulikuwa tunapewa fedha  ambayo tujipanga tufanye na matumizi mengine pia tumefundishwa matumizi ya kompyuta, sisi tunaenda kusoma Afrika Kusinitunaenda kuwa sehemu ya kutimiza malengo ya dira 2050,”alisema Malaika.