WAKANDARASI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA NJE YA NCHI

Na Aziza Masoud,Dar es Salam

WAKANDARASI  nchini wametakiwa kuacha kulalamika badala yake kufanya kazi kwa bidii,weledi katika miradi wanayopewa nchini ili serikali iweze kuwasaidia kupata za miradi ya nje ya nchi

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti  24,2024 na Mwenyekiti wa Bodi  ya Nishati Vijijini (REB)  Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu  katika kikao chakutambua wakabdarasi waliofanya vizuri katika Mradi wa Kupeleka Umeme maeneo ya Pembezoni mwa Miji Awamu ya Tatu (Peri Urban III) inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Amesema lengo la REA kupitia miradi hiyo  ni kuwatengeneza  wakandarasi wazawa kuwa mahili,kutekeleza miradi kwa weledi,ubora na wakati ili badae  wakandarasi hao waweze kutekeleza na miradi ya nje ya nchi.

“Tukaze buti tuondokane na kulalamika,changamoto mnazozipata  ziwafanye kuwa imara nawaona mkifika mbali kabisa,kesho yenu ni nzuri,kupitia miradi hii ya REA  itawatoa nchini na kuwapa miradi  nje ya nchi.

“Serikali haitashindwa kuwatafutia kazi wakandarasi kwenda nje ili  muendelee  kuimarika na kufanya kazi na kufanya kazi kwa bidii,” Balozi Meja Jenerali Mstaafu Kingu.

Amesema kumekuwa na wakandarasi  mbalimbali nchini ambao wanatakeleza miradi ya maendeleo huku akitolea mifano wa nchi za China,India na Tunisia na kubainisha kwamba  uwepo  wao katika nchi mbalimbali unatokana na uzalendo waliouonyesha katika nchi zao hivyo kutoka nje ya nchi inawezekana kama kila mtu atafanya kazi kwa bidii.

Awali akizungumzia kuhusu tuzo hizo,Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan, Saidy alisema utendaji madhubuti (Performance) na kukamilisha Miradi ya PERI Urban III kwa wakati kumechangia Wakandarasi hao kupewa tuzo hizo.

“Kipekee, niwapongeze Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwasimamia Wakandarasi wazawa kwenye Miradi ya PERI Urban III na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati. Natambua kuwa ninyi ndio mlio kuwa Washauri Elekezi wa mradi huu, hivyo mnao mchango mkubwa katika mafanikio haya”. Amekaririwa Mhandisi Saidy.

Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa REA iliahidi kuwa kwa sasa, itaanza kuwatunuku tuzo na vyeti kwa Wakandarasi wanaofanya vizuri kwenye usambazaji wa nishati ya umeme vijijini.

“Tuliahidi na sasa tumetimiza, tumeona hii ni njia nzuri ya kuwafanya waongeze nguvu, kwenye utekelezaji wa Miradi ya usambazaji wa nishati ya umeme vijijini, wale wanaofanya vizuri basi tuwatambue”. Amesisitiza Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi, Hassan Saidy.

Kwa upande wa Mwakilishi kutoka Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB); Mhandisi, Gloria Simbakali ameipongeza REA kwa kuwaalika ili kushiriki hafla hiyo lakini pia amepongeza kwa hatua ya utoaji wa tuzo kwa Wakandarasi waliofanya vizuri kwa jukumu moja wapo la CRB ni kuratibu zoezi la usimamizi pamoja na uwajibikaji (Performance) kwa Wakandarasi (Wanachama). 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO); Mhandisi, Robert Semsela ameipongeza REA kwa kutekeleza na kuendelea kuwafikia Wananchi wengi kupitia Miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini na kuongeza kuwa lengo ni kuboresha maisha ya Watu wa vijijini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *