Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ametoa rai kwa sekta binafsi nchini Tanzania kujiandaa na kuyapokea mageuzi makubwa yanayofanywa kwenye sekta ya madini ili watanzania washiriki kikamilifu kwenye uchumi huu.
Mavunde ameyasema hayo leo Agosti 26,jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na kituo cha Televisheni cha Clouds wakati akielezea mikakati mbalimbali ya Wizara ya Madini.
“Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan ameelekeza utekelezaji wa sheria na sera za madini kuwezesha kundi kubwa la Watanzania kushiriki na kunufaika na sekta ya madini.
Tunahimiza viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa zenye ubora na shindani zinazohitajika migodini ili kupunguza uagizwaji wa bidhaa nje ya nchi.
Lengo letu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma za migodini barani Afrika,tuna eneo la ulipokuwa mgodi wa Buzwagi sasa litagawiwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini.
Kwasasa baadhi ya wawekezaji wa nje wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini wameanza kufungua viwanda Tanzania kwenye eneo hilo la Kahama kwa sharti kwamba lazima waingie ubia na Watanzania.
Kiasi cha fedha kilichotumika kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwenye manunuzi ya bidhaa na huduma ni Trilioni 3.1.Hizi ni fedha nyingi sana na lazima zibaki hapa nchini na watanzania kunufaika badala ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi.”Alisema Mavunde
Kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini Sura ya 123 imetambua rasmi ushiriki wa Watanzania kwenye uchumi wa Madini na hivyo kutoa fursa ya Watanzania wengi kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi huu.