NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Marekani imesisitiza nia ya kushiriki katika kuendeleza Mradi wa Kabanga Nickel na Kampuni ya BHP.
Pia imeweka mkazo wa ushiriki wake katika mradi huo wa kimkakati ambao ni kati ya miradi mikubwa na kielelezo katika sekta ya madini nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambae amefanya mazungumzo na kampuni ya Tembo Nickel ambayo Serikali ya Tanzania ni Mbia ili kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Kampuni mama ya Tembo Nickel pamoja na Serikali ya Marekani kupitia kwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania Balozi Battle na ujumbe wa Marekani uliobebwa na Helaina Matza,Mratibu Maalum wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa Ajili ya Mpango maalum wa Nchi saba zilizoendelea zaidi Kiuchumi duniani G7.
Katika ujumbe huo uliowasilishwa Matza umebeba malengo ya kuwezesha miradi mbalimbali ya kimkakati (PGII) na pia unathibitisha kuwa nchi ya Tanzania ni nchi inayovutia wawekezaji na mazingira ya uwekezaji ni rafiki na hii imechochewa sana falasafa ya uongozi wa Rais Samia Hassan ya 4R-Reconciliation(Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga upya).
Akizungumza katika mkutano huo Waziri Mavunde ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuimarisha zaidi uhusiano na Marekani ambao ndio umeleta mafanikio haya.
“Mafanikio haya yanatokana na mikakati ya Mh. Rais katika mashauriano yake kwenye Mkutano wa Marekani na Afrika uliofanyika mwaka 2022 na pia ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris wakati wa ziara yake Tanzania mwezi Machi 2023,” amesema.
Aidha, Mavunde alipata wasaa wa kukutana na Afisa Mkuu wa Maendelezo wa Kampuni ya BHP , Catherine Raw aliyekuja nchini kutizama maendeleo ya Mradi wa Kabanga Nickel na kuisisitizia Serikali ya Tanzania nia ya kushiriki katika kuendelea Mradi huu ambao unaenda sambamba na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha madini kitakachojengwa Wilayani Kahama,Mkoa wa Shinyanga uwekezaji utakaogharimu zaidi ya Dola Milioni 500.