Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa amesema mahitaji ya mabasi ya mwendo kasi kwa njia za Ubungo na Mbagala ambayo barabara yake imeshakamilika ni zaidi ya 670 na kuitaka Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) kuhakikisha wanakamilisha idadi hiyo kabla ya Desemba mwaka huu.
Mchengerwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizindua mageti janja na kadi za janja na Wakala wa Mabasi Yaendeyo Haraka ( DART) amesema kwa sasa kumekuwa na uhitaji mkubwa wa mabasi yaendayo haraka na kusisitiza kwamba endapo wahusika wataona hawatakuwa na uwezo wa kununua magari hayo watafute wazabuni wazawa ambao watasaidia kuongeza magari hayo.
Amesema mahitaji ya huduma yamekuwa makubwa na kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 80 mpaka 90 ya wakazi wa Dar es Salaam wanatamani kutumia mabasi ya mwendokasi lakini inashindikana kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za huduma na uchache wa magari.
“Kutokana na umuhimu wa usafiri huu ,kumekuwa na uhitaji mkubwa wa mabasi ambapo kwa sasa yanahitajika mabasi 170 katika njia ya Mbezi wakati njia ya Mbagala ikihitaji zaidi ya mabasi 500,Udart hakikisheni mabasi yamepatikana kabla ya Desemba.
“Ongezeno ubunifu wakaribisheni watanzania kuwa mzabuni ili kushirikiana na serikali waweze kuwahudumia watanzania,hakuna sababu yakufikiria watu wa nje wakati watanzania wapo,mbona mabasi ya mikoani yapo miaka yote yanamilikiwa na Watanzania,”amehoji Mchengerwa.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa kadi janja amewaagiza watendaji wa Dart kutoka maofisini ili waweze kusimamia huduma za mabasi hayo.
Amesema uzinduzi huo wa mageti janja na kadi janja unatokana na maendeleo ya teknolojia na kufanya huduma hiyo iwe ya kiwango cha juu.
“Niwapongeze kwakutekeleza maelekezo mliyopewa na kamati ya bunge,mfmo huu utafanya abiria kuachana na matumizi ya tiketi za karatasi,unajibu hoja za wananchi katika changamoto za ulipaji nauli .
“Kabla ya hapo wananchi walikuwa na malalamiko mengi,wapo waliokuwa wanalalamikia kuhusu chenji zao,mtu anatoa fedha anaambiwa chenji hamna kadi hizi zitaondoa changamoto hii,”amesema Mchengerwa.
Amesema ni vema kuhakikisha kadi janja hizo zinapatikana kwa urahisi ili kusiwe na changamoto na wananchi wafurahie huduma hiyo.
“ Mkaongeze ufanisi ili kila mwananchi anayetumia afurahie,nafahamu kwa sasa tunajipanga kwemda kwenye majiji mengine lakini kabla ua hapo lazima tumalize changamoto za Dar es Salaam,tunataka kwenda Dodoma ,Mwanza,Mbeya na Arusha,”amesema.
Awali Mtendaji Mkuu wa Dart,Dk.Athumani Kihamia amesema uzinduzi wa mageti janja na kadi janja hizo una faida nyingi ikiwemo kupunguza foleni katika vituo.
“Uzinduzi kadi janja na geto janja utasaidia kupunguza foleni kwa abiria,kuondoa uchafuzi wa mazingira kutokana na karatasi za tiketi pia zitaondoa udanganyifu kwenye mapato,”amesema Kihamia.