Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limezindua msimu wa nne wa kampeni ya ‘Twenzetu Kileleni’ huku wakihimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupanda Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara Tanapa Jully Lyimo alisema kampeni hiyo ni sehemu ya kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika katika sura ya utalii.
“Tunafahamu kuwa kila ifikapo Desemba 9 nchi yetu huadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika, kama Tanapa tumekuwa tukitumia siku hii kutangaza utalii wa hifadhi ya taifa ya Mlima wa Kilimanjaro, watanzania waende kupanda,”alisema.
Alisema upandaji huo ulianza tangu mwaka 1961 wakati nchi ikipata uhuru ambapo ambapo Kapteni wa Jeshi la Wananchi wakati huo Alexander Nyirenda alipandisha mwenge kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Lyimo alisema zoezi hilo liliendelea likiongozwa na viongozi wakuu wa Jeshi la Wananchi akiwemo Jenerali mstaafu Mrisho Sarakikya na baadaye Jenerali Mstaafu George Waitara.
Katika sura ya Utalii, TANAPA imekuwa ikitumia fursa hii ya maadhimisho ya siku ya uhuru kuhamasisha watanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kutangaza vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hii kupitia kampeni ya ‘Twenzetu kileleni’ .
“Lengo la kampeni hii ni kuhamasisha Watanzania kupanda mlima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika,”amesema Kamishna Lyimo na kuongeza..
“Nichukue nafasi hii kuwahamasisha Watanzania wenzangu kushiriki upandaji huu ikiwa ni kuonyesha uzalendo na kupenda vivutio vyetu.
Amesema mwaka huu ni msimu wa nne wa kampeni hiyo ambapo wanatoa hamasa kwa watu binafsi, watanzania ndani na nje ya nchi, mabalozi, taasisi za Serikali na binafsi kujitoa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizi.
“Kama tulivyofanya mwaka jana jumla ya kampuni tatu ndio zimejitokeza kushiriki kampeni hii katika msimu huu wa nne Kampuni hizo ni ZARA Tours, African Zoom na African Scenic,”amesema Kamishna Lyimo.
Amesema kampuni ya ZARA TOURS itatumia njia ya Marangu kama ilivyozoeleka, African Zoom watatumia njia ya Machame na African Scenic watatumia njia ya Lemosho ambapo idadi ya siku za kupanda mlima huo ni 6 kwa njia ya Marangu.
“Utaratibu utakuwa siku saba kwa njia ya Machame na kwa Lemosho itakuwa siku 8 huku Gharama za kupanda mlima zitakuwa ni shillingi 1,55,000/- kwa njia ya Marangu, shillingi 1,830,000/- kwa njia ya Machame na 2,000,000/- kwa njia ya Lemosho aliongeza Kamishna Lyimo
Naye Afisa Uhifadhi Mkuu Mapinduzi Mdesa kutoka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliwataka watanzania wote kujitokeza katika kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika pamoja na kushiriki katika juhudi za kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro
“Kama mwenyeji wa mlima niwakaribishe watanzania kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika lakini tunajukumu la kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro kwa kustawisha uoto wa asili kwenye maeneo yetu”
Aidha, Mdesa aliongeza kuwa tafiti zinaonyesaha kuwa chanzo cha barafu kuyeyuka Mlima Kilimanjaro ni uwepo wa pepo kavu zinazotokea baharini na maeneo mengine ya nchi zikifika kwenye ile barafu ya Mlima Kilimanjaro zinapelekea Barafu ile kupungua ukubwa wake na kutoa rai ya kukijanisha Tanzania kwa kupanda miti ya asili ili pepo zinazotoka kwenye fukwe ziende na unyevu na kusaidia barafu iendelee kuwepo.
Historia inaonyesha kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961. Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kille cha Mlima Kilimanjaro.
Tukio hili limekuwa likihusisha kikundi cha wanajeshi wachache wakishirikiana na askari wa Hifadhi za Taifa Tanzania kwa utaratibu wa kampuni ya utalii ya ZARA ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita maadhimisho haya yalipata sura mpya ya ushiriki wa wananchi na kutambulika kwa jina la “Twenzetu Kileleni” ambapo kwa sasa ni msimu wa nne.