Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua rasmi Onesho la nane la Swahili International Tourism Expo _S!TE (S!TE 2024) ambalo linatarajia kufanyika jijini Dar es Salaam.
Onyesho hilo lenye lengo la kutamgaza utalii nchini linatarajia kuanza Octoba 11 hadi 13 Jijini Dar es salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru amesema lengo la onesho hilo ni kuwakutanisha watoa huduma waliopo katika mnyororo wa thamani wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
“Onesho la S!TE linalenga kuutangaza utalii wa Tanzania katika nyanja za kimataifa ambapo watoa huduma kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kuonesha bidhaa mbalimbali za utalii sambamba na kutengeneza mtandao wa biashara,” amesema Mafuru.
Amesema Onesho hilo litaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Explore Tanzania For a life Time Investment and Seamless Tourism Experience” ikiwa kama mwendelezo wa programu ya Tanzania the Royal Tour iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilipo nchini.
Amesema Onesho hilo litakwenda sambamba na utekelezaji wa sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 pamoja na mkakati wa kutangaza utalii kimataifa (2020-2025) ambayo imetilia mkazo kuitangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii.
“Onesho hili pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano III( FYDP III 2021/22_2025/26 ambalo zao la utalii wa mikutano na matukio (MICE Tourism) limeanishwa kama zao la utalii la kimkakati kwa lengo la kufikia watalii millioni tano na mapato ya Dola za Marekani Billioni sita ifikapo mwaka 2025,” amesema.
Amefafanua kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuutangaza utalii inayolenga kuvutia watalii wengi kutembelea Tanzania pamoja na kukuza uwekezaji katika sekta ya utalii.
Aidha amesema Onesho hilo linatarajia kuhudhuriwa na waoneshaji wa bidhaa na huduma za utalii zaidi ya 120 sambamba na wanunuzi wa bidhaa na huduma za utalii (International Hosted Buyers) takribani 120 kutoka Nchi ambazo masoko ya kimkakati ya utalii ikiwemo Asia, Ulaya na Amerika.
Ameongeza kuwa, Onesho hilo litahusisha utangazaji wa bidhaa mbalimbali za utalii, jukwaa la uwekezaji, semina kuhusu masuala ya utalii na masoko na mikutano ya wafanyabiashara za utalii.
“Onesho hili pia litafuatiwa na ziara za mafunzo (FAM trips) ambazo zinalenga kuwajengea uelewa wanunuzi wa bidhaa na huduma za utalii kuhusu vivutio vya utalii ili waweze kuvitangaza katika Nchi zao na Dunia kwa ujumla.
“Kwa mwaka huu ziara hizo zimejikita katika kufungua Kanda za utalii zinazochipukia ikiwemo ukanda wa utalii Magharibi na ukanda wa utalii Kusini sanjari na kufungamanisha shughuli za utalii zinazofanyika Zanzibar na Tanzania Bara,” amesema Mafuru.
Aidha ametoa rai kwa wadau wa utalii waliopo ndani na nje ya nchi hususani wakala wa biashara za utalii, watoa huduma za malazi, wakala wa safari, waongoza watalii na Mashirika ya usafiri wa anga kushiriki na kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zinazotokana na Onesho la S!TE 2024.