NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM
Wananchi 1,865 wa Mtaa wa Kipunguni Kata ya Kipawa wanaotakiwa kuhama kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wamemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan wakiomba walipwe fidia zao.
Wananchi hao awali walifanyiwa tathmini mwaka 1997 na tangu wakati huo wamekuwa wakisubiri kulipwa fidia kupisha upanuzi huo.
Wakizungumza Septemba 13,2024 wakati wa mkutano wa hadhara uliohitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala na kufanyika katika Kata ya Kipawa wamesema maisha yao yamekuwa ya taabu huku wakiwa hawajui hatima yao.
“Wana Kipunguni tunateseka, maisha yetu yako hatarini nyumba zimebomoka watu wamekimbia, hata ikitokea ukavamiwa na kupiga kelele hakuna anayekusaidia.
“Mume wangu amenikimbia, nina watoto sita sina mwelekeo, tunakuomba mama Samia tusaidie tuweze kupata haki yetu,” amesema Saada Ndimgwango mkazi wa Kipunguni Mashariki.
Mkazi mwingine wa Kipunguni, Emmanuel Gama, amesema wamekuwa wakipata ahadi nyingi lakini mpaka sasa hakuna malipo yoyote yaliyotolewa.
Naye Aseri Simon amesema; “Novemba mwaka jana tulikuja ofisini kwako (kwa Mkuu wa Wilaya) na tulikwenda hadi bungeni kwa Waziri Mkuu kwa suala hili hili je, serikali itakuwa tayari kulipa asilimia 21 ya usumbufu iliotusababishia?
Akijibu hoja za wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Rais Samia ameshatoa maelekezo na kwamba mwezi ujao watalipwa.
“Tunachosubiri sasa ni mifumo ya namna gani fedha hizo zitalipwa, lakini ni ndani ya mwezi wa kumi. Jumanne (Septemba 17) saa mbili asubuhi mje ofisini mpate uhakika,” amesema Mpogolo.
AHADI ZA MALIPO
Julai 7,2023 Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliwahakikishia wananchi hao kuwa watalipwa fidia kabla ya Oktoba 2023 kwa kuwa fedha zipo na kwamba Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 143.9.
Alisema fedha hizo zitalipwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/24.
Aidha Julai 8,2024 Dk. Nchemba alitoa ahadi nyingine kuwa watalipwa fidia hizo Agosti 2024.
Mwigulu alitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Liwiti, baada ya kutakiwa na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Amos Makala, kutoa majibu ya suala hilo.