Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
SERIKALI imevipongeza vyama vya siasa nchini kwa kuendelea kulinda amani na umoja vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu William Lukuvi alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha kwenye vyama vya siasa baada ya kuteuliwa na Rais Dk.Samia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Amesema umoja na amani utaendelea kuimarika ikiwa kila chama cha siasa kitafuata falsafa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kutaka maridhiano,,ustahimilivu,mabadiliko na kujenga upya.
“Umoja na amani uliopo ndio unaosababisha viongozi wa Serikali kutembelea vyama vya siasa na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo ndani ya nchi.
“Wanasiasa ndio kila kitu kwa wananchi hivyo endeleeni kutunza amani ili Tanzania iendelee kusonga mbele kwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli,”alisema Lukuvi.
Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu Lukuvi alisema Rais Dk.Samia amehagiza chaguzi hizo zitakazofanyika ziwe za uhuru,heshima na haki kwa faida ya watanzania wote.
“Nawahakikishieni uchaguzi wa mwaka huu utaenda vizuri kwa kufuata Sheria na kanuni zilizowekwa alisema,”alisema.
Lukuvi alisema Serikali imejipanga kwa kila atakayechaguliwa na wananchi na kupata kura nyingi huyo ndiye atakaye tangazwa mshindi kwa wananchi.
” Kwenye mashindano yeyote ni lazima kuwepo na ushindani hivyo hata uchaguzi wa mwaka huu na mwaka ujao lazima mshindi atapatikana bila ya kujua atatoka chama gani,” alisema.
Hata hivyo katikà ziara hiyo Lukuvi alivisihi vyama vya siasa nchini kuacha kuwa na siasa za mihemko na badala yake wafanye siasa zenye hoja na maelewano.
“Rais Dk.Samia ameniagiza chaguzi za mwaka huu ziwe na mfano kwa sababu anazitaka ziwe na utulivu na ustahimilivu,’alisema.
VYAMA VYA SIASA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kutembelewa na Waziri Lukuvi viongozi hao waliihakikishia Serikali kuwa kutakuwa na uchaguzi wa utulivu kwa lengo la kulinda amani ya nchi.
“Chama chetu Cha UDP sera yetu kubwa ni upendo na tunajua kuwa siasa si uadui na tutahakikiaha salsafa za Rais Dk.Samia zinatuongoza vyema ,”alisema Mwenyekiti John Cheyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR_MAGEUZI Joseph Selasini alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha chaguzi za mwaka huu zinaenda vizuri huku wakiwahamasisha wanachama wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katikà daftari la wapiga kura litakaloanza Novemba 11 mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama Cha wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba alisema anaishukuru Serikali kwa kuleta falsafa ya 4R ambayo ndani yake kuna maridhiano.
“Naona 4R zimeshaanza kufanya kazi yake hadi leo hii Waziri anatembelea vyama vya siasa ofisini kwao hayo ni mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya siasa,”alisema Lipumba.
Ziara ya Waziri Lukuvi ambayo ametembelea vyama vya siasa 19 vilivyokuwa na usajili wa kudumu ilianza juzu,jana ametembelea vyama vinne vya CUF,UDP,NCCR-MAGEUZi na NLD.