BWAWA LA NYERERE KUONGEZA UZALISHAJI KUFIKIA MEGAWATI 900

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

SERIKALI imesema mradi wa kuzalisha Umeme wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unatarajia kuongeza uzalishaji kutoka megawati 700 za sasa mpaka 900 za umeme  ndani ya muda mchache ujao.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa umeme wa Kanda ya Kusini mwa Afrika Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu, Dk. Khatibu Kazungu mbali na mrafi huo wa JNHPP vipo vyanzo vingine vya kuzalisha umeme. 

Amesema vyanzo hivyo ni pamoja na  mfumo wa jua ambao kwa sasa unauwezo wa kuzalisha Megawati 600 huku kwa kutumia joto ardhi wanauwezo wa kuzalisha megawati 5000 za umeme.

“Kwa hiyo tupo vizuri kama nchi na mahitaji ya umeme yapo vizuri, sasa ni suala la kujipanga sisi kama Serikali hasa kujua tunawezaje kutumia vyanzo hivi vingine ili kuongeza megawati za umeme katika Taifa letu,” amesema Kazungu

Aidha amesema Tanzania kuna mradi mwingine ambao unaitwa Gridi Imara ambao una lengo la kuboresha miundombinu ya umeme pamoja na kuendeleza vyanzo vipya ili kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo muhimu  kila sehemu ya nchi.

Akizungumzia kuhusu kikao hicho, amesema lengo kukutana na wataalamu hao wa masuala ya umeme kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni kujaribu kuweka mikakati ili kuona ni kwa namna gani wataweza kutumia vyanzo vya umeme vya pamoja na kushirikiana hasa katika kufua, kusafirisha na kusambaza umeme kwa wateja.

“Sisi Serikali tuna mradi mkubwa wa usarishaji umeme unaitwa TAZA, mradi huu unakusudia kuunganisha miundombinu ya umeme kati ya Tanzania na Zambia, hivyo tunapokutana katika vikao kama hivi tunajaribu kupitia mikakati hiyo pamoja na hatua tulizozifikia,” amesema

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) anayeshughulika na uzalishaji umeme, Costa Rubagumya amesema kikao hicho kimehusisha wakurugenzi wa nishati ya umeme kutoka nchi wanachama wa SADC ambazo zinaunganishwa na miradi mbalimbali ya umeme.

Amesema kupitia mkutano huo unatoa fursa kwa nchi wanachama kuwapa uwezekano wa mauziano ya umeme kati ya nchi ambazo zipo upande wa Southern na East Power Pool kwa Tanzania.

“Faida kubwa ya kuwa na mashirikiano haya ni uwezekano mtu mmoja akiwa na shida mwingine anamsaidia, ushirikiano tunaoupata utatusaidia kuwa salama katika umeme na ulinzi wa nishati hii,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa hilo la wadau wa Umeme Kanda ya Kusini mwa Afrika, Steven Diwa amesema wadau hao wanapaswa kuendeleza ushirikiano katika umoja huo kuhakikisha nchi zao zinakuwa na mpango sahihi wa upatikanaji wa umeme.

Amesema changamoto wanazokabiliana nazo ni nyingi, lakini pia zinafungua fursa za ukuaji na ushirikiano na kwamba moja ya sababu kuu za kufurahia mkutano huo ni kukutana wakati ambapo Tanzania inafanya maendeleo makubwa katika kuunganishwa umeme kikanda.

“Uunganisho wa umeme na Kenya upo karibu kukamilika, na uunganisho na Zambia unakuja hivi karibuni. Tunatarajia kwa hamu kuwaona Tanzania wakiingia kikamilifu kwenye mtandao wa umeme wa kikanda.

“Kama kanda, macho yetu yako kwenye Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere na uwezo mkubwa wa nishati utakaotolewa. Tunatazamia kuona sehemu ya nishati hiyo ikisambazwa kwa nchi za kusini mwa Tanzania na kwingineko, ambayo haitaleta tu mapato zaidi kwa Tanzania, bali pia itatoa fursa za kujifunza kwa Tanesco kuhusu jinsi ya kuendesha mifumo mikubwa ya umeme iliyounganishwa,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *