SILAA MGENI RASMI  MKUTANO MKUU WA TEF KESHO

Na  Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa anarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano Mkuu wa nane wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Novemba 06, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema katika mkutano wanachama 130 kati ya 167 waliopo mchi nzima wamethibitisha kushiriki.

Amesema mkutano huo ambao unaanza kesho Alhamisi Novemba 07 hadi 09, 2024, jijini Dar es Salaaam utakuwa na kauli mbiu ya ‘Weledi wa kitaaluma kwa uhimilivu wa vyombo vya Habari’.

“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Waziri Silaa kukutana na watu wa vyombo vya Habari tangu alipoteuliwa nafasi hiyo. Pia kwenye mkutano huu atakuwepo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

“Pia katika mkutano huo tutajadili na kuingiza wanachama wapya 25, maombi ni mengi tunachambua vigezo vya uzoefu na kiwango cha elimu ambacho ni Shahada ya kwanza na awe amefanya kazi kuanzia miaka 10,” amesema Balile.

Amefafanua kuwa, kutakuwa na mada kuu mbili, ikiwemo kuhusu utendaji wa vyombo vya Habari na uchumi wa vyombo vya Habari.

“Tutaangalia katika mwaka huu mzima tangu umeanza ni mambo gani yametokea kwenye taaluma yetu, tumefanya jambo gani ambalo ni zuri kama waandishi wa Habari, tumepatia wapi na tumekosea wapi. Kwa maana tusipojitathimini hatuwezi kujua kama tunakwenda vizuri au hatuendi vizuri.

“Mada ya pili tutaangalia uchumi wa vyombo vya Habari, tunajua mwaka huu Juni iliwasilishwa taarifa ya hali ya vyombo vya habari mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwahiyo tunakwenda kuangalia vyombo vyetu vina hali gani kwasasa, tufanye nini kuimarika zaidi na jambo zuri ambalo tumesema tuanze nalo wahariri ni tuache kulialia,” amesema na kuongeza:

“Hatutabadilisha hali zetu kwa kila siku kulia hadharani, tufanye kazi kubadili hiyo hali mbaya kuwa hali nzuri, tunavyo vyombo vya Habari ambavyo vinafanya vizuri na kulipa watu wake vizuri, kulipa bima kwahiyo tutabadilishana ujuzi. Na kwa kweli kwasasa tumeazimia badala ya kutoka hadharani kwamba vyombo vya Habari vina hali mbaya, bali tujitokeze hadharani kunadi mikakati ili vyombo hivi vifanye biashara pasipo kila siku kilio ni kile kile,”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *