Na Mwandishi Wetu,Bariadi
KAMPUNI ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Safi Tanzania (REA) wamezindua rasmi mradi mkubwa ambao utawafikia na kuwawezesha wafanyakazi wote wa Magereza kuacha matumizi ya mkaa na kuni na kuhamia matumizi ya gesi.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Julai 1,2025 katika gereza la wilayani Bariadi mkoani Simiyu ambapo kupitia mradi huo Oryx Gas imewwzesha upatikanaji wa mitungi ya kg 15 na majiko ya sahani mbili pamoja na viunganishi vyake kwa punguzo kubwa ambapo REA wao wamewalipia askari na maofisa kwa niaba ya Serikali.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa Miradi Safi ya Kupikia kutoka Oryx Gas Tanzania LTD Peter Ndomba amesema pia kampuni hiyo kwa kushirikiana na msambazaji wake mkuu wa mkoani Simiyu wametoa punguzo la kudumu kwa kila askari aliyenufaika na mradi huo.

“Mtungi wa gesi unapoisha atajaziwa tena kwa bei nafuu.Punguzo hilo la kujaza gesi litaendana na kupelekewa nyumbani mara gesi inapoisha.Ugawaji wa mitungi umeenda sambamba na utoaji wa elimu ya matumizi salama ya gesi.
“Hii ni utekelezaji wa sera ya kampuni ya Oryx Gas ya kutoa mafunzo ya matumizi salama ya gesi kwa kila mtumiaji wa mtungi wa Oryx,siku zote tumekuwa tuhakikisha mtumiaji wa mtungi wa gesi ya Oryx anakuwa salama na katika hilo tumekuwa tukitoa elimu ya matumizi salama ya gesi na tutaendelea na utaratibu huu siku zote.”
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi.
“Mei 8, 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Toka kuzinduliwa kwa mkakati huo, Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuokoa mazingira pamoja na vifo vilivyokuwa vinatokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi na salama ya kupikia.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya Oryx Gas Kilogramu 15 na majiko ya gesi ya sahani mbili 330 imegawiwa kwa Watumishi wa Magereza Mkoa wa Simiyu.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Simiyu, SACP Lugano Msomba ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Oryx Gas kuwawezesha Watumishi wa Magereza kupata nishati safi ya kupikia na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa wengine katika kampeni hiyo.
