FCC KUENDELEA KUIMARISHA MAZINGIRA YA WAFANYABIASHARA NCHINI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaa.

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Hadija Juma Ngasongwa amesema taasisi hiyo  imekuwa ikisimamia wawekezaji wa ndani ya nchi kupitia sheria madhubuti  zinazosimamia uwekezaji ili kusaidia kuimarisha sekta ya biashara nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Julai 4,  2025 katika banda la FCC katika  Maonesho ya 49 ya  Kimataifa  ya Biashara  Dar es Salaam (DTIF)  maarufu kama Sabasaba alisema  tume hiyo  ipo kwa ajili yakufuatisha maono ya Rais Dk.Samia Suluhu  Hassan yakuimarisha hali ya biashara nchini.

“Lengo la kuanzishwa  tume ya ushindani ni kusimamia na kuimarisha ufanyaji wa biashara nchini, kulinda  walaji dhidi ya mienendo potofu ya hali ya ufanyaji biashara nchini kati ya kampuni na kampuni, pamoja na kudhibiti bidhaa bandia,”alisema Hadija.

Alisema pamoja na kuljnda walaji pia wana jukumu la kuhakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hivyo mwekezaji wa ndani ya nchi anapofaya biashara anatambua kuwa kuna sheria za kusimamia uwekezaji zinawalinda.

” Tunajivunia na tunashukuru sana serikali kuweza kutengeneza mazingira sahihi ya wawekezaji kuhakikisha kwamba mwekezaji wa ndani  anazifikia fursa zinazopatikana nchini na mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara,”alisema.

Alisema katika maonesho hayo ambayo yamewakutanisha wafanyabiashara zaidi ya 3000 anaamini kuwa yatawakutanisha wafanyabishara na watu tofauti tofauti kwa lengo la kubadilishana mawazo.

 Pia aliwakumbusha wafanyabiashara kuhusu sheria kudhibiti bidhaa bandia amapo  ni kosa la jinai kujihusisha na bidhaa bandia hivyo wananchi wafike kwenye banda lao ili kupata elimu na  waweze kutofautisha bidhaa bandia na halisi.