WANAWAKE,VIJANA WATAKIWA KUJUSAJILI Na MFUMO WA NeST

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imewahamasisha Watanzania, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kujisajili kwenye mfumo wa manunuzi ya kielektroniki wa Serikali (NeST) ili kunufaika na zabuni za asilimia 30 zilizotengwa kwa ajili ya makundi maalum

Akizungumza Julai 5, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba, amesema tayari zabuni zenye thamani ya Shilingi Bilioni 16 zimeshatolewa kwa makundi maalum, huku lengo kuu likiwa ni kufikia thamani ya Shilingi Trilioni 5.

“Tumesema taasisi zote za ununuzi zitenge asilimia 30 kwa makundi maalum. Na huu ni wakati sahihi zaidi kwa Watanzania kujitokeza kwani mwaka mpya wa fedha umeanza, na tenda nyingi zimetangazwa tayari kupitia NeST,” alisema Simba.

Ameeleza kuwa mfumo wa NeST unapatikana kwa urahisi kupitia intaneti na kila Mtanzania mwenye sifa anaweza kufuatilia tenda zote za Serikali moja kwa moja.  

“Miaka 20 iliyopita watu hawakujua tenda ya Serikali inapatikana vipi. Leo ukiwa na bando lako tu, unafungua NeST, unaona kila tenda ya Serikali iliyotangazwa,” alisema.

Amehimiza vikundi vya sanaa na wajasiriamali kujisajili kwa kuandaa Katiba ya kikundi, leseni halali, na nyaraka muhimu nyingine.  

Aidha, amesema kwa wale wasioweza kufika Sabasaba, PPRA imefungua ofisi za kanda sita kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa karibu.

Simba amesema NeST ni suluhisho la uwazi, ushindani na fursa halali kwa Watanzania wote hivyo hakuna sababu ya kukosa zabuni kama vigezo vinakidhiwa.