Na Aziza Masoud,Dar es SalaamSHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeibuka mshindi na kupewa tuzo ya kuwa na mchango mkubwa katika kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DTIF) maarufu kama Sabasaba.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TPDC, Maria Mselemu, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya utendaji kazi wa hali ya juu na ufuatiliaji makini wa shughuli za shirika hilo.

“Hii ni tuzo yetu ya tano katika maonesho haya, na kwetu sisi imekuwa kawaida kupata tuzo kutokana na ubora wa huduma na miradi yetu, ikiwemo tuzo ya mazingira tuliyopokea leo,siku zote tunajivunia kuwa taasisi kinara linapokuja suala la utunzaji wa mazingira,”alisema Mselemu.
Aliongeza TPDC imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa ukaa kwa kutumia nishati safi ya kupikia na ile inayotumika katika magari, hatua ambayo imechochea mafanikio yao katika nyanja za mazingira.

“Kupitia matumizi ya nishati safi, tumeweza kuondoa zaidi ya tani 100,000 za hewa ukaa. Hii ni hatua kubwa katika kulinda mazingira yetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza Mselemu.
Maonesho ya Sabasaba yanayofanyika kila mwaka katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, yanawakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali za biashara na maendeleo, yakilenga kuonyesha bidhaa na huduma bora kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.
