Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI ya awamu ya sita imeongeza fedha za kuwezesha elimu bure katika Mkoa wa Mara kutoka shilingi bilioni 5.6 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 7.5 mwaka wa fedha 2025 kwa shule za msingi na kutoka shilingi bilioni 6 hadi bilioni 12.85 mwaka 2025 kwa shule za Sekondari.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Evans
Mtambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na ongezeko la shule, wanafunzi na maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.
Alisema kuwa jumla ya shule mpya za msingi 20 na sekondari 27 zimejengwa katika Mamlaka za Serikali ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara ambapo hadi sasa Mkoa huo umepokea shilingi bilioni 4.1 ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ya Mkoa shilingi bilioni 1.6 na ujenzi wa Shule tano za Sekondari za Amali za Halmashauri kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2.9.

“Katika kuimarisha elimu ya ufundi nchini, Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi Tanzania (VETA) imejenga vyuo vitano vya ufundi katika Wilaya za Butiama, Rorya, Serengeti, Tarime na Bunda kwa gharama ya shilingi bilioni 12.71,” alisema.
Aliongeza kuwa ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Butiama umekamilika na mafunzo yameanza kutolewa na vyuo vinne vingine unaendelea.
Kanali Mtambi aliongeza kuwa
katika sekta ya elimu, Serikali ya Awamu ya Sita imekarabati majengo ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Butiama (MJNUAT), Kampasi ya Oswald Mangombe kwa jumla ya shilingi bilioni 2.66 na kukiwezesha Chuo kuanza kudahili wanafunzi kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 baada ya mradi huo kukwama kwa takribani miaka 15.
Alifafanua kuwa ujenzi wa miundombinu mipya ya chuo hicho katika Kampasi ya Butiama unaendelea kwa shilingi bilioni 102.5 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
“Ujenzi wa mradi huu upo katika hatua za ukamilishaji na utakiwezesha Chuo kudahili wanafunzi 1,100 kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026 katika programu mpya 11,” alisema.
Akizungumzia Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi alieleza kuwa katika Uwezeshaji huo Serikali imetoa miongozo ya kuyawezesha makundi mbalimbali katika jamii kuweza kuimarisha uwezo wao wa kushiriki shughuli za maendeleo na kuleta usawa wa kiuchumi katika jamii.

“Katika kipindi hiki, kuna ongezeko la vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri za Mkoa wa Mara kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka vikundi 187 mwezi Novemba, 2020 hadi vikundi 324 Aprili, 2025,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa fedha zinazotolewa kama mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.63 Novemba 2020 hadi shilingi bilioni 5.88 mwaka 2025.
Mkuu wa Mkoa huo alifafanua kuwa kumekuwa na ongezeko la vikundi vya wanawake kutoka vikundi 92 Novemba, 2020 hadi 99 Aprili, 2025; vikundi vya vijana kutoka 53 hadi 139 na vikundi vya watu wenye ulemavu kutoka 42 hadi 86.
Alisema mafanikio yaliyopatikana kutokana na vikundi hivyo ni pamoja na kuongezeka kwa ajira, uchumi wa vikundi, mtu mmoja mmoja na kupunguza utegemezi wa makundi hayo katika jamii.
