SH BILIONI 69.75 KUHUDUMIA MIRADI YA AFYA SIMIYU

Na Asha Mwakyonde,DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Simiyu
Anamringi Macha ameeleza kuwa
katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 umepokea jumla ya shilingi bilioni 69.75 ambapo shilingi bilioni 26.80 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Afya huku shilingi bilioni 10.96 ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na Shilingi Bilioni 31.99 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Hayo yaliyasema jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alisema mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya ni pamoja na kuongeza kwa Zahanati kutoka 190 mwaka 2020 hadi 242 mwaka 2025,
Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 10 mwaka 2020 hadi 21 mwaka 2025.

Alisema nyumba za watumishi wa Afya zimeongezeka kutoka 175 mwaka 2020 hadi 252 mwaka 2025 na kwamba bajeti ya dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za Afya imeongezeka kutoka Bilioni 4.9 mwaka 2020 hadi 8.2 mwaka 2025.

“Upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za Afya umeongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2020 hadi asilimia 93 mwaka 2025,” alisema.

Aliongeza kuwa magari ya kubebea wagonjwa yameongezeka kutoka Magari matano mwaka 2020 hadi magari 15 mwaka 2025 pamoja na
magari ya usimamizi wa shughuli za Afya yameongezeka kutoka magari matano mwaka 2020 hadi Magari 13 mwaka 2025.

Mkuu wa Mkoa huo alieleza kuwa Watumishi wa kada ya Afya wameongezeka kutoka watumishi 1,723 mwaka 2020 hadi 2,168 mwaka 2025 sawa na asilimia 25.

Alisema serikali imekamilisha ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Bariadi, Itilima na Busega na ukarabati wa Hospitali kongwe Tatu ambazo ni hospitali ya Halmashauri ya Mji Bariadi, Maswa na Meatu.

Macha alisema serikali imekamilisha ujenzi wa majengo mawili ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na Hospitali ya Wilaya Meatu.

Alisema serikali imekamilisha ujenzi wa majengo manne ya huduma za dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na Hospitali za Halmashauri za Bariadi, Maswa, na Itilima.

Macha alifafanua kuwa katika jitihada za Serikali kuimarisha utoaji wa huduma za Afya Mkoa umepokea vifaa tiba mbalimbali ambavyo ni :- CT SCAN, X – Ray za kisasa Sita (6), utrasound Machines Saba na dental chair za kisasa 13, mashine za X-Ray Sita na mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 80 hadi 100 kwa siku.

Alieleza kuwa Mkoa umeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo wagonjwa waliohudumiwa wameongezeka kutoka 7,000 mwaka 2020 hadi 35,636 mwaka 2024.

Macha alisema serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.044 ambalo lina uwezo wa kubeba jumla ya vitanda 140 vya kutolea huduma.