Na Asha Mwakyonde, DODOMA
AFISA Uhusiano kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Renatus Sona ameeleza kuwa mchango wa wakala huo katika Sekta ya kilimo Uvuvi na Mifugo ni mkubwa kutokana na miradi ambayo wameitekeleza, kuendeIea kuitekeleza katika maeneo hayo.
Hayo ameyasema leo Agosti 3,2025 katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji ‘Nane nane’ ambayo yanafanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nzuguni jijini hapa
amesema wanashiriki maonesho hayo kwa sababu kuna miradi ambayo wameifanya katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo.

SEKTA KILIMO
Amefafanua kuwa katika miradi ya kilimo TBA imetekeleza na kusimamia ujenzi wa vihenga na maghala ya kuhifadhi chakula katika mikoa nane Tanzania Bara ambayo ni Dodoma,Shinyanga, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Manyara, Njombe na Songwe.
Sona ameongeza kuwa mradi huo umejengwa na kampuni kutoka nchini Polandi ambapo TBA ndio wasimamizi wa mradi na kwamba umekamilika na tayari umeshaanza kufanya kazi.

“Mradi huu umekuwa na tija kubwa katika uhifadhi wa chakula umebuniwa na kujengwa vizuri pamoja na kutekelezwa vizuri, sisi TBA tumeusimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo na umeshakamilika unafanya kazi, tunajivunia kwa kushiriki kama wasimamizi ndio maana tupo kwenye maonesho ya nane nane kuwaambia wananchi wanaotembelea banda letu TBA tunatekeleza miradi katika sekta ya kilimo amesema.
SEKTA YA UVUVI
Akizungumzia miradi ya uvuvi, ameeleza kuwa TBA imebuni na kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo Mkoa wa Mtwara katika Bahari ya Hindi eneo la Msimbati ambapo imejengwa mabwawa ya kufugia samaki kupitia maji chumvi.
Sona ameongeza kuwa ni mradi ambao unaendelea na kwamba utakapokamilika utakuwa na tija katika sekta ya uvuvi na kuinua kipato cha wafugaji wa samaki huku akisema mbalimbali na Mkoa wa Mtwara mradi huo huo unafanyika katika Dar es Salaam eneo la Kunduchi.

SEKTA UFUGAJI
Amesema wakala huo umefanya ubunifu na kutekeleza ujenzi wa mradi wa soko la mnada wa mifugo huku akisema wanatambua sehemu maarufu ya kuuzia na kununua mifugo kwa wafanyabisahara wa mifugo ni mnada.
“Mradi tumeubuni sisi TBA katika eneo la Buzirayombo mkoani Geita , tunaendelea kuutekeleza hivyo wafanyabisahara wa mifugo watafanyabiashara katika eneo zuri na litavutia wateja,” amesema Afisa huyo.
Ameongeza kuwa katika Sekta hizo Wakala huo umejipambanua na umekuwa na mchango mkubwa na kwamba miradi hiyo itachangia kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi.

TBA ni taasisi ya serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Ujenzi na kazi kubwa inazozifanya ni kusimamia na kuendeleza miliki za serikali kwa maana ya majengo, nyumba pamoja na viwanja ambavyo ni mali ya serikali na kutoa ushauri kuhusiana na ujenzi.

