Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imezindua matumizi ya teknolojia mpya ya vipimo vya vinasaba (DNA) kwa ajili ya kubaini visumbufu mbalimbali vinavyoathiri uzalishaji wa mazao nchini, ikiwemo magonjwa na wadudu waharibifu.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza duniani kuingiza teknolojia hiyo katika sekta ya kilimo.
Hayo yamesemwa leo, Agosti 6, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, wakati wa maonesho ya wakulima na wafugaji ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kuzindua teknolojia hiyo, Profesa Ndunguru amesema kuwa teknolojia hiyo ya kisasa inaweza kutoa majibu ndani ya dakika 20, moja kwa moja shambani, bila kuhitaji kwenda maabara.
“Leo hii katika viwanja vya maonesho ya Nane Nane, tumezindua teknolojia mpya ya vipimo vya vinasaba (DNA), ambayo itasaidia kutoa majibu ya haraka kuhusu visumbufu vinavyoathiri mazao hapa nchini, vikiwemo magonjwa na wadudu waharibifu,” amesema.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa mazao yanayozalishwa nchini yanakidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuongeza fursa za soko la nje kwa wakulima wa Tanzania.
“Teknolojia hii itawezesha wakulima kuwa na uhakika wa kufanya biashara na mataifa ya nje, jambo litakaloongeza pato la taifa na kipato kwa wananchi kwa ujumla,”amefafanua Prof. Ndunguru.

Ameeleza kuwa licha ya matumizi yake katika sekta ya kilimo, teknolojia hiyo pia inaweza kutumika katika sekta nyingine kama mifugo, afya ya binadamu, na uhifadhi wa anwani, na hivyo kuwa teknolojia yenye manufaa makubwa kwa Watanzania.
Aidha, amewakaribisha wadau wa mbegu, miche, pamoja na wananchi kwa ujumla kutembelea ofisi za TPHPA ili kupata huduma, ambapo teknolojia hiyo itawawezesha kubaini ubora wa mbegu wanazotumia.
