Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), KUNJE NGOMBARE MWIRU, akiongozana na Mgombea Mwenza Chimu Abdallah Juma JUMA, leo Agosti 9, 2025, wamehitimisha zoezi la uchukuaji wa fomu kwa siku ya leo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Kunje amesema kuwa chama chao kitajikita zaidi kwenye uzalendo kama msingi wa maadili ya uongozi na maendeleo ya Taifa.

“Vipaumbele vya chama chetu ni vitatu Uzalendo, uzalendo na uzalendo, ” akisisitiza.
Akifafanua zaidi, Kunje amesema kuwa mihimili mikuu ya dola Bunge, Mahakama na Serikali inahitaji uzalendo ili kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Ni kwanini nimetaja mara tatu? Kwa sababu Bunge linataka uzalendo, Mahakama inataka uzalendo, na Serikali inataka uzalendo. Vingine vyote vitafuata baadaye,” ameeleza.
Amefafanua kuwa hatua inayofuata baada ya kuchukua fomu, wanatarajia kuanza safari ya kutafuta wadhamini katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Visiwani kama taratibu za kisheria zinavyoelekeza.
“Nina zoezi la kupata wadhamini 2000, wadhamini 200 kwa kila mkoa kutoka mikoa minane ya Tanzania Bara, mkoa mmoja Unguja na mkoa mmoja Pemba. Safari bado ni ndefu, lakini tuko tayari,” amesema.
Aidha, Kunje ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi nzuri ya kuratibu na kuandaa mazingira bora ya kuchukua fomu.

“Nimeridhika na uandaaji wa tume, sasa naenda kutembea mikoa 10 kwa ajili ya kutafuta wadhamini,” ameeleza mgombea huyo.
Kunje na msafara wake walifika katika Ofisi za Tume majira ya saa 9:19 alasiri na walihitimisha mchakato huo saa 9:57 alasiri, wakiwa wameambatana na wanachama wengine wa chama hicho.


