LATRA YAANZA KUTOA VIBALI VYA USAFIRI WA WAYA KWA LENGO LA KUCHOCHEA UTALII

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo, amesema mamlaka hiyo imeanza kutoa vibali kwa ajili ya usafiri wa waya katika maeneo mapya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza shughuli za utalii nchini.

Akizungumza Agosti 8, 2025, katika kilele cha Maadhimisho ya Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, CPA Suluo alisema kuwa usafiri wa waya ni moja ya maeneo mapya ambagyo yamejumuishwa rasmi kwenye sheria za usafiri, na sasa taratibu zote za kisheria zimeshakamilika.

“Eneo hili la usafiri wa waya lilikuwepo kisheria, lakini kulikuwa hakuna kanuni za kulisimamia. Kwa sasa, kanuni zimekamilika na zipo kwenye hatua za mwisho kabla ya kusainiwa na kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndipo tutaendelea kutoa leseni,” alieleza CPA Suluo.

Alisema kuanza kutolewa kwa vibali hivyo kutawapa fursa wawekezaji kuingia kwenye sekta ya usafiri wa waya, hali itakayochochea utalii wa ndani na wa kimataifa, pamoja na kuongeza pato la taifa.

Akizungumzia ushirikiano wa LATRA na Shirika la Reli Tanzania (TRC), alisema jukumu la mamlaka hiyo ni kuhakikisha miundombinu yote ya reli, pamoja na mabehewa na vichwa vya treni vinavyotumika, vinakidhi viwango vya usalama kabla ya kuanza kutumika.

“Kama ambavyo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa inasimamia ubora wa barabara, nasi tunahakikisha miundombinu yote ya reli, mabehewa na vichwa vya treni vinavyonunuliwa kutoka nje ya nchi vinakaguliwa kwa kina kabla ya kutumika. Tunatoa ithibati ya usalama kwa TRC kuendelea kutoa huduma,” alifafanua.

Aliongeza kuwa LATRA huwatuma wataalamu wake kukagua mabehewa na vichwa vya treni vinavyotengenezwa nje ya nchi kabla havijaletwa, ili kuhakikisha vina ubora unaohitajika kwa matumizi ya hapa nchini.

Kuhusu usafiri wa mabasi ya hadhi ya juu (luxury buses), CPA Suluo alibainisha kuwa LATRA haihusiki kupanga nauli ya mabasi hayo kwa kuwa yanashindana katika ubora wa huduma. Hata hivyo, mamlaka hiyo inapanga nauli kwa madaraja ya kawaida na ya kati ili kuhakikisha huduma ya usafiri inapatikana kwa Watanzania wengi.

“Jukumu letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya usafiri kwa gharama nafuu. Ndiyo maana tunapanga nauli kwa mabasi ya kawaida na ya kati ili wananchi wengi waweze kumudu,” alisema.