MUNIR ZAKARIA: SIYO DHAMBI FAMILIA ZA VIONGOZI KUGOMBEA UONGOZI

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Munir Zakaria, amekemea vikali dhana inayojengwa na baadhi ya watu kwamba familia za viongozi wakuu wa nchi hazina haki ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ubunge.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 17, 2025, Zakaria amesema dhana hiyo ni ya kupotosha na inapingana moja kwa moja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatambua haki ya kila raia kuchagua na kuchaguliwa.

“Kwa mujibu wa Katiba, kila Mtanzania ana haki ya kuchaguliwa na kuchagua. Siyo haki kusema kwamba mtoto au mwenza wa kiongozi hastahili kugombea. Dunia nzima kuna mifano ya familia zinazorithi majukumu ya uongozi kwa mafanikio makubwa,” amesema Zakaria.

Ametolea mfano Marekani, ambapo familia za kisiasa kama ya Kennedy na Bush zimetawala siasa kwa miongo kadhaa.

“Familia ya Kennedy ilitoa viongozi maarufu kama Rais John F. Kennedy na Maseneta Edward na Robert Kennedy. Hii inaonesha jinsi familia moja inaweza kuwa na mchango mkubwa katika siasa ya taifa,” amesema.

Ameitaja familia ya George Bush kama mfano mwingine wa mafanikio ya urithi wa kisiasa, pamoja na Bill Clinton ambaye mke wake Hillary Clinton aligombea urais na pia alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya Barack Obama.

“Kwa hiyo, siyo sahihi kuamini kwamba urithi wa uongozi kwa njia ya kifamilia ni jambo baya. Badala yake, ni baraka, ni faida na ni nguvu ya kuendeleza taifa. Tukubali ukweli kwamba familia zenye historia ya uongozi zina mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa,” alisisitiza Zakaria.

Akizungumzia malalamiko ya upendeleo katika mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea ubunge ndani ya CCM, Zakaria amesema madai hayo si ya kweli na yanalenga kukichafua chama.

“Mchakato wa uteuzi ulifanyika kwa haki na uwazi. Wengi wa walioteuliwa ni watu wa kawaida wasio na mizizi ya muda mrefu ndani ya chama. Hii inaonesha kuwa hakuna upendeleo wowote,” amesema.

Ameongeza kuwa yeye binafsi hajawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini, hadi Mei mwaka huu alipojiunga rasmi na CCM, na mwezi mmoja baadaye kuchukua fomu ya kuomba uteuzi kupitia Jimbo la Chamanzi.

“Nilikuwa mwandishi wa habari kwa zaidi ya miaka 15. Kati ya wagombea 15 katika jimbo langu, majina saba yalipitishwa na mimi nikiwemo, bila kuwa na ‘baba’ wala ‘mama’ ndani ya CCM. Huu ni ushahidi kuwa chama kimezingatia haki na usawa,” amesema.

Kuhusu kauli za aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kuwa utaratibu wa kumpata mgombea urais na mgombea mwenza haukufuatwa, Zakaria amesema kauli hizo hazina msingi kwani sera ya CCM ni ya kuendeleza Muungano wa serikali mbili, huku Polepole akiwa ni muumini wa serikali tatu.

“Ni ajabu kwamba wakati akiwa msemaji wa chama, aliukalia kimya ukiukwaji wa taratibu mbalimbali, lakini leo anaibuka na kukosoa kila jambo. Wakati wake kulikuwepo na malalamiko ya uchaguzi, kuvamiwa kwa maduka ya fedha, kufungwa kwa akaunti za wafanyabiashara, ukandamizwaji wa demokrasia, pamoja na kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na kurusha kwa moja kwa moja vikao vya Bunge – yote haya hakuyasema,” alisema Zakaria.

Amesema ni muhimu kwa viongozi waliowahi kushika nyadhifa nyeti kuonyesha mfano wa kuigwa kwa kuwa wa kweli na waadilifu hata wanapostaafu nafasi hizo.