Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
NCHI za Afrika zimetakiwa kuungana ili kuwa na nguvu moja yakupambana na mifumo iliyowekwa na nchi za Magharibi kwa ajili yakujinufaisha kiuchumi na kusababisha migogoro baina ya viongozi na wananchi wa nchi hizo kwa kiasi kikubwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwanajumui wa Afrika na Mwanafalsafa kutoka Zimbabwe, Dk. Joshua Maponga, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari 22, 2026.

Alisema nchi za Afrika kumekuwa na migogoro baina ya wananchi hasa vijana na viongozi hivyo ni wakati wa kundi hilo kutambua kuwa adui wao mkubwa si watu waliopo madarakani, bali ni mifumo iliyopandikizwa na nchi hizo kwa lengo la kunufaika na rasilimali za Afrika.
“Naona nchi za Afrika vijana wamekuwa wakipambana na serikali na kuilalamikia lakini wanashindwa kugundua tatizo sio serikali ila mifumo iliyowekwa na watu wanaojinufaisha kupitia nchi zetu,kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikitumika kama msingi wa uchumi wa mataifa ya Magharibi,”alisema Dk.Maponga.

Alisema ili kuondoka tatizo hilo ni wakati wa nchi za Afrika kuamua kuungana ili kuweza kupambana na nchi za ughaibuni kwakuwa wamekuwa wakiharibu na kusababisha vurugu katika maeneo ambayo yana rasilimali na kuleta migogoro.
Amesema sasa ni wakati wa Waafrika wenyewe, hususan vijana, kuamka kiakili, kuacha maisha yasiyo halisia na kuelewa kuwa umoja na kufanya kazi kwa pamoja ni silaha muhimu katika kulijenga bara lenye mshikamano na maendeleo ya kweli.

“Vijana, kama mngeruhusiwa kuchukua serikali kama mnavyotaka, je, mnaweza? Je, mna uwezo wa kuendesha taifa, au hii ni hasira tu inayotokana na mifumo ya uchaguzi isiyokidhi ndoto ya mustakabali tunaoutaka?” alihoji Dk. Maponga.
Alisisitiza kwa kusema kuwa vijana wanapaswa kujiuliza ni mustakabali gani wanaoutaka kwa Afrika na ni kwa njia gani watahakikisha ndoto hiyo inafikiwa.
“Huu ni wakati wenu na nafasi yenu ya kubadilisha historia na kuunda Afrika ya kesho. Tambueni kuwa matatizo ya Afrika ni matatizo ya Tanzania pia. Tunapaswa kuacha kufikiria kuwa tuko katika nchi tofauti, bali tuko katika nchi moja iitwayo Afrika, yenye mikoa tofauti. Tanzania ni mkoa mmoja tu, kama ilivyo Zimbabwe, Uganda, Kenya na mingine,” alisema.

Aidha, Dk. Maponga amesema ndoto ya Afrika yenye umoja iliyoanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere inawahitaji vijana wa sasa kuisimamia na kuitimiza.
“Kazi na maisha ya Mwalimu Nyerere yalionesha mwanzo wa ndoto ya Afrika moja. Juhudi zake hazikuishia Tanzania pekee, bali zilienea hadi maeneo mengine ya bara. Rafiki yake wa karibu, Hayati Kwame Nkrumah, naye alikuwa sehemu ya waasisi wa ndoto hii ya Afrika huru na iliyoungana,” aliongeza.
Hata hivyo, Dk. Maponga alisisitiza kuwa Tanzania imekuwa nguzo muhimu ya harakati za ukombozi barani Afrika, akisema bila mchango wa Tanzania kusingekuwepo mataifa huru kama Afrika Kusini, Zambia, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji, Uganda na Kenya.


