TCAA INAVYOENDELEA KUPAMBANA NA UHABA WA MARUBANI WAZAWA

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

TAKRIBANI vijana 23 wamepata udhamini wa kusomea masomo ya urubani kupitia Mfuko wa Mafunzo wa  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania  (TCAA Training Fund)  huku wanne kati yao  na  wameshaajiriwa  na mashirika mbalimbali ya ndege yaliyopo nchini.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA),Salim Msangi ametoa takwimu hizo jana wakati  akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu marubani  hao sambamba na kuelezea shughuli mbalimbali zilizofanywa wakati wa kuadhimisha waliomaliza masomo yao chini ya ufadhili wa mfuko huo na maadhimisho ya siku ya  Usafiri wa Anga Duniani ambayo huadhimishwa Kimataifa kupitia Shirika ya Usafiri  wa Anga  Duniani (ICAD).

Amesema wahitimu hao ni sehemu ya marubani  603 waliopo nchini ambapo kati yao ni wazawa ni 344 huku 259 wakiwa ni raia wa kigeni.

Amesema hatua hiyo ni muendelezo wa kupambana na uhaba wa marubani ambao  wanaingia sokoni na kuajiriwa katika makampuni ya ndege nchini.

“Huu ni muendelezo wa serikali katika kusomesha marubani kwakuwa tunakua watu wanapenda kusoma masomo haya ila wanashindwa kwa sababu ya gharama,serikali imeamua kugharamia ili kukidhi uhaba wa marubani wazalendo uliopo katika kada hiyo na kukuza sekta ya usafiri wa anga,”amesema.

Amesema mchakato wa masomo  wa marubani hao ulianza mwishoni mwa mwaka 2019 ambapo marubani hawa walipelekwa masomoni chuo cha East African  Civil Aviation Academy kilichopo Uganda .

“Kuanzisha kwa mfuko huu wenye lengo la kufadhili mafunzo ya urubani na uhandisi wa ndege ambao unasaidia kwa kiasi kikubwa watanzania kusomea fani hizo kwani mafunzo hayo ni gharama na watanzania wachache wanaweza kuyamudu huku kusaidia watanzania kuingia katika soko la ajira kutokana na upungufu  wa watanzania kwenye kada hiyo.

“Marubani hao walijiunga na Chuo cha Mafunzo cha Mosswood Transport Tanzania kwa mafunzo ya Mult -Engine Instrument Rating (MEIR)mnamo Mwezi Julai 2023 na wamemaliza mafunzo hayo na wamefuzu kuwa marubani wa ndege za kubeba abiria yaani Commercial Pilot Licence with Instrument Rating and Multi -Engine Rating,”amesema.

Amesema mnamo mwaka 2022 mfuko ulipeleka mhandisi mmoja katika chuo cha Ethiopia  Academy nchini Ethiopia  ambaye nae amemaliza masomo yake na mwaka 2023 walipelekwa wahandisi wengine 10 amabo hivi sasa bado wanaendelea na masomo na wanatarajiwa kumaliza masomo yao machi 2025.

Msangi ameipongeza kamati inayosimamia mfuko huo kwa kazi nzuri waliofanya hadi kufikia kuwapata vijana hao huku akiwapongeza vijana hao kwa juhudi walizozifanya hadi kumaliza mafunzo yao.

“Natoa wito kwa wadau wetu hasa wanaochangia katika mfuko wa mafunzo kuwasiliana na Mamlaka ili kuwawezesha kuwapatia marubani hao fursa za ajira,”amesema.

Akiongelea wiki ya Usafiri wa Anga Duniani amesema katika kuadhimisha  wiki hiyo  mamlaka hiyo kupitia kitengo cha uhusiano na mawasiliano pamoja na wataalam wake kutoka idara mbalimbali imeweza kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kujenga uelewa  juu ya kazi za Mamlaka katika kuelekea miaka 80 ya usafiri wa anva Duniani.

Amesema pia waliweza kutembelea baadhi ya shule za sekondari zilizopo mkoa wa Dar es Salaam  kwa lengo la kuelimisha na kuhamasisha wanafunzi waliopo mashuleni kusoma kwa bidii na kuweza kuingia kwenye sekta ya anga nchini.

“Pia tulipata fursa ya kufanya semina kwa njia ya mitandano ikiwa na ujumbe wa meet the professionals of aviation lengo ni kuzungumzia  maendeleo mbalimbali yaliyofikiwa katika sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *