Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
CHUO Kikuu Cha Dodoma(UDOM) kinatarajia kuzindua kampasi mpya mkoani Njombe ambapo inatarajia kujikita zaidi katika maeneo ya misitu na kilmo kwa lengo la kufungua ajira katika eneo hilo na mikoa ya jirani.
Akizungumza katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango na Utawala,Profesa Wineaster Anderson amesema chuo hicho ambacho ni miongoni mwa vyuo ambavyo vinatekeleza mtaala wa mafunzo ya amali kupitia kampasi hiyo wataweza kuwasaidia wananchi kutatua changamoto zilizopo katika eneo hilo.
“Tunaenda kufungua kampasi mpya katika eneo letu la Njombe,kule tutajikita katika eneo la misitu,na sote tunatambau Njombe ni misitu ,Njombe ni kilimo lakini kule na mikoa inayozunguka kuna madini na eneo la uvuvi,tunapozungumzia habari ya chuo kutatua changamoto za wananchi mfano mzima itakuwa ni pale kampasi ya Njombe ambapo tutaenda kutatua changamoto za ajira,” Profesa Wineaster.
Amesema kampasi hiyo ambayo itafungua ajira na kutoa ujuzi inatarajiwa kufunguliwa Septemba 2026 kwa sasa ipo katika hatua ya manunuzi ya ujenzi.
Aidha Profesa Wineaster pia amewataka wananchi kutembelea banda lao lililopo ilikuweza kuona taifiti bidhaa walizokuja kuzionesha
“Mwaka huu tumekuja na bidhaa mpya kuwaonesha Watanzania kwa sababu mwaka jana tulikuwa na bidhaa tofauti, nyingine tumeziongeza mwaka huu kuanzia aina za mashine ambazo zinasaidia katika sekta ya samaki. Lakini wanafunzi wetu wameingia katika uwanja wa kutengeneza ‘rockets’ na kwenye maeneo ya vyakula ili kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia lishe asili”.
“Udom inajipambanua kwa kuangalia matatizo ya jamii ya Watanzania na kutumia akili za wanafunzi na wafanyakazi wake kuangalia namna ya kuzitatua hasa katika eneo la afya, teknolojia na ukija Sabasaba utaziona,” amesema Profesa Wineaster.
Amesema bidhaa hizo ambazo zimetengenezwa na wanafunzi mbalimbali wa chuo hicho zinatokana na tafiti walizofanya pamoja na wanataaluma na kusisitiza ndizo zinazowezesha kuwepo kwa teknolojia mpya.
“Bila tafiti huwezi kuja na tekolojia mpya, huwezi kuja na ubunifu wowote kwahiyo tumejipambanua katika eneo hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto ya rasilimali fedha kweye tafiti lakini tunaendelea kujitahidi katika eneo hilo…kikubwa tafiti zetu zimejikita katika jamii ya Watanzania na kutatua matatizo yaliyoko katika jamii yetu Tanzania,” amesema.