Kairuki: Tangazeni bidhaa za mianzi ni fursa kiuchumi

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Anjellah Kairuki ameutaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TGS) kutanganza fursa mbalimbali za zao la mianzi ambalo kwa sasa lina uhitaji mkubwa kwenye masoko ya nje.

Kairuki ameyasema hayo mapema hivi leo Julai 05, 2024 mara baada ya kutembelea Banda la TFS lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Kairuki aliipongeza TFS kwa namna inavyotimiza majukumu yake ya  uhifadhi wa rasilimali misitu na nyuki pamoja na utalii ikoloji na kuutaka Wakala huo kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi lakini pia kutangaza fursa mbalimbali walizonazo.

Aliongeza kuwa utangazaji wa shughuli hizo ni vyema ukawa endelevu hata baada ya maonesho ya Sabasaba kuisha.

“Nimevutiwa na bidhaa hizi za mianzi! Zitangazeni ili wananchi wazijue hii itasaidia kuona fursa mbalimbali zitokanazo na mazao ya misitu  ili waweze kujiongezea kipato”, amesema.

Mapema mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilizindua mkakati wa kitaifa wa mianzi na mpango kazi wake wa Mwaka 2023-2031.

Akizindua mkakati huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki alisema Serikali imeweza mazingira wezeshi ili  kupitia mianzi nchi iweze kupata

kodi na kuongeza fedha za kigeni huku wananchi watakaopanda mianzi wakipata huduma muhimu za kijamii, kujiongezea kipato na ajira za kudumu.

Wakati huohuo, Waziri ametoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho ya Sabasaba hususan Banda la Wizara ambalo liko na taasisi zake zote kuhakikisha inatoa elimu ya uhifadhi lakini pia kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutoa ofa mbalimbali za kutalii.

“Tunao TFS wanaozalisha miche miche ya matunda na mengineyo, ukifika bandani utapata ushauri na miongozo bora, wakakujuza wapi utapata mbegu na miche yetu ya asili lakini na ile ya Kibiashara, amesema Kairuki.

Aidha, Waziri amewakumbusha wananchi kutumia fursa hii ya elimu ya upandaji miti ili kuongeza kiwango cha upandaji miti na kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kukua vizuri.

Maoneshya ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea katika Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar Es Salaam kuanzia tarehe 28 June 2024 hadi tarehe 13 Julai 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *