Zaidi ya watu 800 wapatiwa huduma  banda la JKCI katika viwanja vya Sabasaba

Aziza Masoud,Dar es Salaam

ZAIDI ya watu 800  wamefika katika banda la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupima  matatizo mbalimbali  ikiwemo moyo,sukari na tiba lishe.

Akizungumza katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba,Daktari wa Moyo  wa JKCIA Dk.Marsia Tillya amesema mpaka juzi Jumamosi banda hilo limeshapima wananchi wapatao 883  ambapo kati ya hao watu 196 walikutwa na tatizo la moyo kufanya kazi.

“Tunafanya vipimo na kuwaona watu tofauti tofauti ,watu wapatao 800 tumewaona,asilimia kubwa wanapewa  elimu ya moyo na lishe,pia kuna wagonjwa milango ya moyo ambao tumewapa rufaa ya kwenda JKCI,”amesema Dk.Tillya.

Amesema mlango  wa moyo unatokana sababu mbalimbali ikiwemo homa pia watu wanavyozidi kuishi kunakuwa na mabadiliko mbalimbali yanayodababisha   mlango wa moyo.

“Kwenye  milango ya moyo wengi wameanzia na tatizo utotoni,kwa sababu yakushindwa kuangalia afya mara kwa mara unakuta mtu anakuja kugundua ukubwani,”amesema Dk.Tillya.

Amesema kwa upande wa watu wenye kisukari wanawapa ushauri na elimi ya namna yakuishi na ugonjwa huo na wengine wanaelekezwa kwenda kwenye kliniki.

Kwa upande wa  Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI Anna Nkinda amesema taasisi inashiriki katika maonesho ikiwa na maabara iliyokidho vigezo vya kimataifa hivyo wanafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya vipimo vya damu.

“Wanaangalia jinsi  moyo  unavyofanya kazi,mfumo wa umeme wa moyo,ushauri wa lishe,vipimo vya sukari,kati ta wagonjwa 800 waliofika hapa mpaka Jumamosi,wagonjwa  212 wamekutwa na umeme wa moyo,

“196 wamekutwa na tatizo la moyo kufanya  kazi huku watu  61 wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo yanayohitaji  kutibiwa kibingwa na wameshapatiwa  rufaa ya kwenda JKCI,”amesema Nkinda.

Amesema wameweka huduma kwa bei ndogo katika viwanja vya Sabasaba ambapo ni nusu ya huduma halisi.

Amesema JKCI pia imeanza kutoa  huduma mpya za tiba mtandao na huduma ya kufuatilia maendeleo ya mgonjwa anayetibiwa akiwa nyumbani kwa kutumia kifaa kijulikanacho kwa jina la DOZEE katika viwanja hivyo.

Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *