Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
Mkurugezi Mkuu Shirika la ndege Tanzania ATCL Ladislaus Matindi amesema kwa sasa wameanzisha huduma ya kumtambua mteja ambae anafanya safari zake mara kwa mara ili aweze kupata ofa ya kupandishiwa daraja la tiketi.
Akizungumza na wananchi kutembelea banda lao la katika maonesho ya 48 ya biashara maaru kama Sabasaba ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ikiwemo ukataji wa tiketi na fursa zinazopatikana katika usafiri wa anga kupitia kwa kutumia shirika hilo kwani mteja huyo anaweza kukata tiketi ya daraja la uchumi na kupanda mpaka daraja la Biashara.
“Umekuwa mpango wetu wa kuwatambua wateja wetu ambao wanafanya safari zao za mara kwa mara kupitia shirika letu anakua anapata aina fulani za upendeleo kuchagua siti kupata huduma ya ziada ya mizigo lakini akiwa pia na pointi nyingi anaweza pia kupata tiketi ya bure”,Amesema.
Akizungumzia kuhusu usafiri wa ndege ya mizigo ametoa rai kwa wafanyabiashara kutumia ndege hiyo katika kusafirisha biashara zao nje lakini pia shirika litawasaidia kuyafikia masoko mengi ya bidhaa zao kwa manufaa ya nchi lakini pia kwa manufaa yao binafsi.
Aidha Matindi amesema ushiriki wao wa maonesho kwa mwaka huu umekuwa wa tofauti sana kwani huduma zote zinazotolewa kwa wasafiri wa anga zimewekwa katika sehemu moja ambapo inamuwezesha mwananchi kuweza kujifunza lakini pia kuhudumiwa akiwa katika sehemu hiyo hiyo.
“Hapa katika banda letu utapata huduma zote(one stop center)kwani watoa huduma wote tupo sehemu moja kwa ajili ya kuwahudumia nitoe rai kwa wananchi kuja hapa kujionea na kupata huduma zetu”,amesema Matindi.
Katika hatua nyingine Matindi ametoa rai kwa wananchi kutembelea banda lao la maonesho ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ikiwemo ukataji wa tiketi na fursa zinazopatikana katika usafiri wa anga.
Matindi amesema zipo fursa nyingi ambazo wamekuwa wakizitoa kwa wateja wao ikiwemo huduma za ukataji wa tiketi na kulipa kidogo kidogo kwani huduma hiyo inamsaidia kupanga safari zake bila kuumia kwa kulipa gharama kubwa kwa wakati mmoja.