Na Aziza Masoud ,Dar es Salaam
IKIWA zimebaki siku mbili kufungwa kwa maonesho 48 ya biashara kimataifa maarufu kama Sabasaba miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa kivutio ni pamoja na maroboti yaliyopo katika viwanja hivyo.
Eneo hilo ambapo kuna maroboti limekuwa kivutio na kusababisha kujaza watu wengi ambapo wapo ambao wanasema maonesho yaongezwe siku huku wakiwataka watu waliopo majimbani kutembeleq maonesho hayo.
Akizungumza katika eneo hilo Valentino Kivike ambaye ni mkazi wa Kigamboni amesema maonesho ni mazuri maroboti yamekuwa kivutio sana.
“Sijawahi kuona hii ni teknolojia ni mpya kwangu,naona yanaweza haya maroboti yanaweza kufaa hata kwenye kazi na mambo mengine.
“Hii inaonyesha wanaweza kufanya kazi yoyote kwa sababu nimeona anaweza kucheza hivyo anaweza kufanya na kazi nyingine,”anasema Kivike.
Amesema amefurahi kuona teknolojia hiyo pamona na vitu mbalimbali vilivyomo ndani.
Naye Janeth Joseph ambaye naye mkazi wa Kigamboni amesema roboti ni kitu kipya anaona ni kama sehemu ya mabadiliko katika maonesho hayo.
“Unajua kuna watu hawaji Sabasaba kwa sababu wanahisi hakuna kitu kipya chakujifunza lakini wanapaswa kujua kuwa ukija huku utapata burudani ,unatengeneza afya ya akili,”amesema.
Amesema ni wakati serikali kutoa nafasi zaidi kwa wabunifu wa stadi za mikono na bunifu nyingine.
Ameiomba serikali kuongeza siku za maonesho kutoka ambapo badala yakumalizika Julai 13 iende hadi Julai 20.
Maonesho ya Sabasaba yalianza rasmi Juni 28 na yatarajiwa kumalizika Julai 13.