DK.BITEKO:WAFANYABIASHARA JIANDAENI KUSHINDANA KIMATAIFA

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

NAIBU Waziri Mkuu Dk.Doto Biteko amesema sera mpya ya Taifa Biashara  ya mwaka 2023 ina lengo la kuwaandaa wafanyabiashara kushindana Kimataifa  hivyo amewataka kujiandaa kuingia katika  ushindani huo.

Dk.Biteko ambaye pia ni Waziri wa Madini ametoa kauli hiyo leo Julai 30 wakati wa uzinduzi wa sera hiyo,alisema  sera hiyo  inawaandaa wafanyabiashara kushindana kimataifa, hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kuisoma kwa umakinj.

“Kila ambaye amejindaa kushindana huyo ndo atakayeshinda ambaye hajajiandaa kushinda atakuwa mlalamishi,jukumu letu ni kuandaa watu wetu kushindana kimataifa kupitia sera hiii.

“Tusijione wanyonge,maana mwisho wa siku aliyejiandaa ndo atakuwa mshindi mwishoni kama Taifa lazima tujiandae,”amesema Dk.Biteko.

Amesema   sera ya biashara ina malengo yakuongeza ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi na kuleta ushindani wa bidhaa za ndani ya nchi.

Dk. Biteko, ametoa  wito kwa sekta zote nchini kusoma na kusimamia Sera Mpya ya Taifa ya Biashara na kuifanyia kazi. 

Amesema  kuwa sera hiyo pia inatakiwa kutumiwa kama nyenzo ya kuondoa vikwazo vya biashara na kuweka mfumo wa sheria unaolenga kuimarisha na kukuza biashara.

“Ofisa wa serikali lazima utambue kuwa heshima yako ya kukaa hapo ofisini ni kuhakikisha umewezesha watu kufanya biashara na kupata faida, siyo kuwakwamisha. Kuna watu ambao kazi yao kubwa ni kukwamisha wengine,” amesema  Dk. Biteko.

Ameongeza  kuwa mchango wa sekta ya biashara kwenye pato la taifa bado ni mdogo, hivyo kuna umuhimu wa kutumia sera hiyo kuhakikisha biashara inarahisishwa na mchango wake unaongezeka kwenye pato la Taifa.

“Watu walilalamikia sana kwamba sera yetu imepitwa na wakati. Sasa baada ya kuifanyia mabadiliko ni muda wa kuonyesha dunia kwamba tumefanya mabadiliko na tunakwenda na kasi ya dunia,” amesema  Dk. Biteko.

Ameeleza   kuwa sera ni nyaraka tu, na kama haitafanyiwa kazi itabaki kama kitabu cha hadithi. Aliwataka maofisa wa serikali kubadilisha mtazamo na fikra zao, na kutekeleza yaliyoandikwa kwenye sera hiyo.

“Hakuna faida ya kuwa na sera nzuri lakini wakawepo maofisa ambao kazi yao ni kukwamisha wafanyabiashara. Tunahitaji sera kuwa kiunganishi baina ya wafanyabiashara na serikali,” amesema  Dk. Biteko.

Amewataka wafanyabiashara wote nchini wafahamu kuwa serikali iko kwa ajili yao na inapenda kuona wananufaika na biashara wanazofanya. Hata hivyo, aliwaonya wale wenye tabia ya kukwepa kodi.

Awali  Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amesema sera hiyo imewezekana kutokana na msaada wa wadau mbalimbali zikiwemo balozi za nchi mbalimbali na kampuni ya Trade Mark Afrika. Alisema wadau wengi wamehusishwa na lengo lilikuwa kupata sera inayoakisi hali halisi ya sasa.

“Wadau wengi sana wamehusishwa na lengo letu ilikuwa kuhakikisha tunapata sera inayoakisi hali halisi ya sasa. Nawapongeza wataalamu wa wizara yangu, wamefanya kazi usiku na mchana na kupitia sera hii tunatarajia kuongeza sana mauzo ya nje ikiwemo masoko ya Afrika,” amesema  Dk. Jafo.

Kwa upande wa Waziri wa Viwanda Zanzibar, Omar Shaban, amesema sera hiyo inaenda kujibu changamoto za ndani na kutatua kero ikiwemo za Muungano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Trade Mark, Elibariki Shammy, alisema miundombinu imeboreshwa kwenye mipaka ikiwemo Tunduma kupunguza foleni na vizuizi vya biashara kwenye korido zinazoathiri biashara.

“Tumepunguza vizuizi vya ukaguzi barabarani kutoka zaidi ya 50 hadi sasa hivi vizuizi ni vitatu tu,” amesema Shammy. 

Aliongeza kuwa serikali inasikiliza sauti ya sekta binafsi na kufanyia kazi, na kujengea uwezo vijana, wanawake, na makundi maalum kwa fursa ambazo serikali inatoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *