Na Nora Damian, Dodoma
Sekteratieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imesema kupitia klabu za maadili zilizoanzishwa katika shule na vyuo mbalimbali nchini wanafunzi wamefundishwa elimu inayohusu uadilifu kwa lengo la kuja kupata viongozi waadilifu.
Katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, sekretarieti hiyo iliambatana na wanafunzi wa klabu za maadili kutoka shule na vyuo mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha uadilifu katika ngazi za malezi.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika maonesho hayo, Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Fabian Mpokela, alisema wamekuwa wakipita katika shule na vyuo kwa ajili ya kuanzisha klabu hizo huku wakishirikiana na walimu na walezi wa wanafunzi husika.
“Tunao mwongozo wa uanzishaji klabu za maadili katika shule na vyuo, tunazo klabu zaidi ya 500 nchi nzima. Tunatarajia baadaye kupata viongozi ambao wamelelewa kutoka katika klabu zetu kwa sababu kiongozi hatumpati tu uko juu lazima apitie malezi,” alisema Mpokela.
Alisema walitumia maonesho hayo kutoa elimu na kutambulisha umma kuhusu huduma wanazitoa, kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma.
“Tumepata mwitikio mzuri, watu wengi wametembelea banda letu na tumepokea maoni mbalimbali ya wananchi kuhusu namna bora ambavyo tunaweza kuboresha maadili kwa viongozi wa umma,” alisema.
Mmoja wa wajumbe wa Klabu ya Maadili ya Chuo cha Mipango Dodoma, Apiamwene Mchopa, alisema katika klabu yao wamekuwa wakielimishana mambo ya kufanya ili kuendelea kuwa na maadili.
“Tunafahamu kwamba chuoni ni maeneo ambayo vijana wengi wanaharibika kitabia kutokana na mmomonyoko wa maadili kwahiyo, kazi kubwa ni kukumbushana mambo gani tuyafanye ili tuendelee kupata elimu tukiwa na maadili,” alisema Mchopa.