Uongozi Jatu PLC waitisha mkutano wa dharula

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
ZAIDI ya wanahisa 10,000 waliopo katika kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (JATU PLC)
wanatarajiwa kushiriki katika mkutano mkuu maalum wa dharula utakaofanyika kwa njia ya mtandao kesho wenye lengo la kuwaizinisha wajumbe wa bodi.

Mkutano huo wa dharura wa JATU utafanyika kwa njia ya mtandao (zoom) kesho utakuwa na agenda zisizopungua 15 unakuja wakati ambao kampuni hiyo inapitia changamoto mbalimbvali ikiwemo ukosefu wa fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu JATU Plc, Mohamed Simbano amesema watu watakaoudhuria kwenye mkutano huo ni wale wote wenye hisa katika kampuni hiyo.

Anasema kwa wanahisa ambao watashindwa kuhudhuria au kuteua mwakilishi watapaswa kutuma fomu za uwakilishi mapema kabla ya siku ya kesho.

“Watakaoshiriki mkutano huu ambao utafanyika kwa njia ya mtandao hapo kesho ni wale wanahisa tu, tunataka wanahisa washiriki kuwapitisha wajumbe wa bodi ili kuruhusu wafanye kazi ya kuweza kuirudisha kampuni yetu kwenye uzalishaji,” anasema Simbano

“Kila mwanahisa wakati wa kuingia katika mkutano huo utakaofanyika kwa njia ya mtandao yaani zoom lazima aandike jina lake sahihi kama linavyosomeka kwenye cheti chake hisa ili uongozi uweze kupitia na kuthibitisha kama kweli ni mwanahisa kinyume na hapo ataondolewa kwenye kikao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu JATU Plc, Mohamed Simbano akizungumza jijini Dar es Salaam leo

“Nia yetu ni njema tunataka kila mtu aweze kushiriki kwakuwa hatutaki mwanahisa yeyote apoteze haki yake ya msingi ya kupiga kura kuchagua wajumbe pindi itakapofika,” anasema Simbano.

Anasema mara baada ya mkutano huo kufanyika na kupata wajumbe wa bodi watakuwa na jukumu la kurudisha kampuni kwenye uzalishaji na ndani ya miezi mitatu wataitisha mkutano mkuu ambao utafanyika katika ukumbi mkubwa hivyo wanahisa wote watahudhuria na kutoa maoni yao.

“Baada ya mkutano wa kesho sasa bodi pamoja na viongozi watakuwa na jukumu la kurudisha JATU kwenye uzalishaji na ndani ya miezi mitatu wataitisha mkutano mkuu ambao utafanyika kwenye ukumbi mkubwa maana tutakuwa na uwezo wa kumudu gharama ndogo ndogo za kila siku katika endeshaji ambazo kwa sasa zimesimama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *