NA MWANDISHI WETU, MOSHI
Wahudumu wa hoteli wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, wamelalamika kuhusu unyanyasaji unaofanywa na waajiri wao.
Kulingana na malalamiko yao, wamekumbwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kunyimwa bima ya afya na kukatwa fedha za mfuko wa Hifadhi ya Taifa (NSSF) bila waajiri kuziwasilisha ofisi husika,jambo walilodai kuathiri maisha yao kwa kiasi kikubwa.
Wahudumu hao wamesema kuwa licha ya kufanya kazi kwa bidii, waajiri wamekuwa wakiwafanyisha kazi saa nyingi bila kuwalipa ziada. Pia, wanakabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi, mazingira magumu ya kazi, na kipato kidogo.
Kwa jumla, kuna changamoto 20 zinazowakabili kiutendaji, ambazo wamewasilisha kwa serikali. Changamoto hizo ni pamoja na kunyimwa nafasi za kuhudhuria semina, waajiri kutolipa mishahara kwa wakati, na kutopewa mikataba kazini.
Hayo yamebainishwa Jana, Juni 29,2024 katika Chuo Cha Misitu na Viwanda (FITI) kwenye hafla ya kufunga mafunzo yanayotekelezwa na Serikali ya kukuza ujuzi kwa wafanyazi na watoa huduma ya Hoteli yenye lengo la kuwajengea uwezo na kukuza weledi kwa watumishi wa tasnia ya ukarimu.
Akisoma risala ya wahudumu hao,mbele ya mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula, Mhitimu wa mafunzo hayo, Gadiel Mbuya ameelezea changamoto za manyanyaso wanayokumbana nayo wafanyakazi kutoka kwa waajiri wao.
“Tunaomba serikali itusaidie kuandika waraka maalumu kwa waajiri wote nchini ili kuwafahamisha mambo muhimu katika sheria ya kazi kwani wengi wa waajiriwa tunateseka kuhudumia baadhi ya huduma ambazo hatukupaswa kufanya”
“Kuna hoteli za Moshi hazina NSSF kwa wafanyakazi,tunakatwa NSSF lakini haziwasilishwi ofisi husika,wafanyakazi wachache tunafanyishwa kazi nyingi na hatuna sehemu ya kulalamika na hatuna bima sasa sijui wanategemea tukatibiwe kwa waganga”? amesema na kuuliza,Mbuya.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi wa Hoteli mkoa wa Kilimanjaro (KHA),Abdi Massawe amesema chama kimekuwa kikikutana na changamoto nyingi ikiwemo mafunzo ya Hoteli yanayotolewa na vyuo mkoani hapa ikiwemo kukosa miundombinu stahiki.
“Baadhi ya waajiri kutothamini taaluma na ujuzi wa wafanyakazi wa Hoteli Hali inayomfanya mfanyakazi wa Hoteli kudharau taaluma yake na kupelekea kufanya kazi ya kutoa huduma chini ya kiwango Kwa kutojiamini kwa sababu ameshindwa kuaminika ” amesema Massawe.
Akijibu baadhi ya changamoto, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Leonard Mapha, amesisitiza umuhimu wa waajiri kuendelea kuchangia katika Hifadhi ya Jamii. Anasisitiza kuwa kuna maisha baada ya kustaafu kazi, na hivyo waajiri wanapaswa kupeleka michango ya wafanyakazi ili waweze kupata mafao yanayowawezesha kuendelea kuishi maisha mazuri.
Akizungumzia mafunzo hayo yaliyodunu Kwa siku sita Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi (KVAU), Amosi Nyandwi, ameeleza kuwa lengo la mafunzo ni kuongeza tija kwa wafanyakazi na watoa huduma katika tasnia ya utalii.
“mishahara inategemea tija. Kwa hiyo, waajiri wanapaswa kuwadai wafanyakazi kuongeza tija ili kufaidika na matokeo bora. Ni jambo la maana kwa pande zote kushirikiana ili kukuza ufanisi katika tasnia hii muhimu” amesema Nyandwi.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula, ametoa hotuba ya kufunga mafunzo hayo kwa watumishi 377 wa tasnia ya ukarimu. Katika hotuba yake, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu ili kushughulikia changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika sekta hii.