Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Watu wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amewataka vijana kushiriki kikamilifu kuhakiki na kutoa maoni katika rasimu ya Dira Ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuweza kupata Tanzania wanayoitaka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kufungua mkutano mkuu wa vijana wa kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,Kikwete alisema vijana wanapaswa kufahamu dira hiyo siyo tu makaratasi pekee badala yake inapaswa kutafsiri Tanzania ambayo wananchi wanaitaka.
“Tujadiliane hili lazima watu wajue kuna maeneo hayapo vizuri kwenye dira hivyo ni nafasi yenu vijana kusema ni maeneo yapi ambayo hayaelezwi vizuri na yanapaswa yaweje ili yaelezeke vizuri,tuangalie mapungufu ambayo yataleta maboresho yatakayoisaidia jamii na si kwa kujiangalia wenyewe wakati mliopo sasa.
“Hichi kitu hatujitengenezei wenyewe tunaitengenezea jamii,watoto tulionalo leo ifikapo 2050 ndiyo watakaokuwa vijana na watatumia dira hii hivyo tuangalie jambo ambalo lina ubora,”alisema Kikwete.
Alisema mbali na dira pua wizara imekuwa ikiratibu utengenezaji wa sera ya vijana ambayo inazungumza mambo mengi ambapo kupitia sera hiyo zipo hatua za msingi zinaweza kufanyika.
“Hiki ndiyo kipindi chakuchambua sera na kuonyesha maboresho kwakuwa Tanzania tunayoitaka inaanza leo,”alisema Kikwete.
Alisema kupitia sera na dira vijana wanapaswa kuangalia vitu vya msingi ikiwemo sekta ya elimu pamoja na masuala ya kinga ya kijamii.
“Nawashauri vijana endeleeni kushiriki kikamilifu katika mijadala ya Kitaifa hasa yenye lengo la kufanya maboresho katika sekta yenu,sisi kama serikali tupo tayari kuwasikiliza maoni yenu na yatafanyiwa kazi,”alisema Kikwete.
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation, Salha Aziz alisema kuelekea 2050 ni muhimu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikaainiaha wazi mikakati mahususi ya kuweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwa na program za kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokwamisha vijana kujiajiri pamoja na ajira kwa vijana.
“Ni muhimu serikali kushughulikia changamoto na malalamiko ya vijana wanaofanya biashara ndogondogo nchini pamoja na wale wanaoanzisha biashara mpya, kwani biashara nyingi zinakutana na vikwazo vinavyokwamisha biashara hizo kuweza kukua,” alisema Salha.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la The African Leadership Initiative for Impact, Joseph Malekela alisema ni vyema Dira hiyo ikaainisha namna ambavyo inawaandaa vijana kuweza kushuka nafasi mbalimbali za kimaamuzi, pamoja na kuwaandaa kuweza kuzitumia nafasi hizo kwa uadilifu na uzalendo.