Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
SERIKALI imewataka wadau kuendelea kutoa maoni yakuboresha rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050 na kuahidi kuyafanyia kazi kwakusimamia utekelezaji wake.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 10, 2025 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji),Stanslaus Nyongo wakati mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKI) wakati wakuhakiki rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema serikali itazingatia maoni yatakayotolewa na kila taasisi kuhakikisha nchi inakuwa na dira inayoeleweka na kutekelezeka.
“Tunavyokusanya maoni katika Dira hii tutazingatia mawazo yanayotolewa na wadau,Dira hii itapelekwa bungeni na itafungwa kisheria ili kuondoa ile hali ya kila kiongozi kuja na mambo yake,”amesema Nyongo.
Amewataka wadau kutokuwa na kuhusu maoni yao kwakuwa wataendelea kushirikiana kutoa maoni na kuyasimamia.
Amesema malalamiko ya awali katika Dira ilikuwa kuhusu lugha ambapo ilitumika lugha ya kigeni ambayo imeshafanyiwa marekebisho na kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili.
Amesisitiza Dira imezingatia sana maoni ya vijana kwakuwa kundi hilo ndilo linahusika zaidi katika kuitumia.
Awali wakitoa maoni ya ziada ya Azaki juu ya dira ya Maendeleo ya Taifa 2050,Deus Kibamba mmoja wa mjumbe wa kikosi kazi cha mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia AZAKI alisema dira hiyo ni nyenzo muhimu kwa upangaji wa pamoja wa ndoto za Watanzania kama Taifa ambapo kupitia Dira, Watanzania wanaweka bayana matarajio na mipango yao juu ya Tanzania waitakayo katika miaka 25 ijayo.
” Imekuwa ni faraja kwetu kama asasi za Kiraia kushirikishwa katika zoezi hili adhimu la kuchangia maoni na mapendekezo yetu kwenye rasimu ya Dira iliyoandaliwa na Kamati maalum ya Kitaifa ya utayarishaji wa Dira ya Taifa 2050.
“Katika kuandaa maoni na mapendekezo yetu, AZAKI tumefanya uchambuzi wa kina wa rasimu ya Dira na kubainisha mambo kadhaa tuliyoamini yanahitaji maboresho,”amesema
Amesema rasimu hiyo ya dira ya taifa imesheheni mambo mengi mazuri ambapo wao kama Azaki wameweza kutoa mapendekezo ya maboresho yanalenga kuifanya rasimu izae Dira iliyo na ukamilifu zaidi.
Amesema ni matumaini yao kuwa uchambuzi, maoni na mapendekezo waliyowasilisha katika waraka huo yatazingatiwa na Kamati na kupewa nafasi katika ukamilishaji wa Rasimu ya Mwisho ya Dira.
Naye Nuru Marwa miongoni mwa mjumbe wa kikosi kazi cha mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia AZAKI, alisema miongoni mwa mapendekezo wanayotoa katika kamati hiyo ni pamoja na kutoshahibiana kwa maudhui pamoja na data kwenye chapisho la Kiswahili na Kingereza.
Akitoa mfano katika aya 2.1 unaoeleza Uchumi Imara, Jumuishi na shindani, aya ya kwanza kwenye utangulizi upo tofauti na chapisho la Kingereza ambapo kasi ya kukua kwa uchumi ni asilimia 6.4 wakati ya kiingereza ni asilimia 5-6.7.
Amesema katika hilo Azaki imependekeza kwamba kamati itumie taarifa na takwimu sahihi na za aina moja kwenye nyaraka zote mbili.
“Katika suala la Utawala na Uongozi bora haujawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi hivyo tunapendekeza, Utawala na Uongozi bora kama moja ya sekta za kimkakati, kwani ukitaka maendeleo unahitaji watu, ardhi, uongozi bora na siasa safi ili kufikia maendeleo tunayotarajia.
Marwa amesema katika Sekta ya Elimu haijawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi wakati dira hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo teknolojia inakua kwa kasi na ndiyo nyenzo kuu ya uzalishaji na tija Katika nchi ambayo idadi kubwa ya watu wako chini ya umri wa miaka 15, matumizi na uzalishaji wao wa kidijitali vinapaswa kuzingatiwa kupita makuzi yao ya kielimu.
Amesisitiza kuwa AZAKI inapendekeza sekta ya elimu kuwa ni moja ya sekta za kimapinduzi ili utekelezaji wa Dira uendane na wakati.
Akizungumzia suala la makadirio ya idadi ya watu ifikapo 2050 kufikia milioni 140 haiendani na takwimu rasmi za Ofisi za Takwimu Taifa (NBS) ambayo inaelezea , malengo ya maendeleo endelevu ya dunia dira ya Afrika Mashariki 2050 na Dira ya SADC ambapo imetajwa ifikapo 2050 idadi ya watu Tanzania itakua imefikia milioni 151.3.
Amesema wao kama Azaki wanapendekeza takwimu hiyo ya makadirio ya idadi ya watu kufikia 151.3 itumiwe na Dira pamoja na makadirio haya ipo haja ya dira kuzingatia hali ya uzazi na ongezeko la watu ambayo imekua ikishuka kwa kasi kwa baadhi ya mikoa.
“Kwakua takwimu zinaonesha utegemezi 87.1 ya waTanzania nitegemezi, Azaki tunapendekeza mikakati na shabaha mahsusi ya kupunguza mzigo wa utegemezi, kwa kuimarisha na kuongeza tija kwenye elimu, ajira, na uzalishaji,2.8 Rasimu ya dira toleo la kiswahili ina mapungufu mengi ya kiuandishi na matumizi ya lugha.
” Azaki tunapendekea uandishi wa Dira toleo la kiswahili uzingatie matumizi sahihi ya lugha adhimu ya kiswahili kwakuwa ndio toleo kuu,”amesisitiza Marwa.
Aidha amesema wanaipongeza serikali kwa utoaji wa Dira kwani imetoa mpango wa utekelezaji ambapo ikifika wakati wa tathmini ya utekelezaji wa Dira ya maendeleo utolewe kupitia data.