NDEGE KUANZA KUTUA IRINGA FEBRUARY 22

Na Mwandishi Wetu,Iringa

WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawawa Uchukuzi

amesema mkoa wa Iringa rasmi utaanza kupokea safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ifikapo Februari 22 mwaka huu baada ya kiwanja cha ndege cha Nduli kukamilika kwa asilimia 93.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo jana alipofanya ziara mkoani Iringa kwa ajili ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Nduli kilichopo nje kidogo ya mji wa Iringa.

” Air Tanzania itaanza kufanya safari zake mara tatu kwa wiki lakini tutaweza kuongeza zaidi ya hapo itategemea idadi ya abiria watakaopatikana,” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha Profesa Mbarawa amesema kuwa mashirika ya ndege ya Pecision Air na shirika la ndege la Auric Air yanatarajiwa kuanza kufanya safari kuanzia mwanzoni mwa mwezi Machi.

Waziri Profesa Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na viongozi wa mkoa kutunza miundombinu hiyo muhimu ili iweze kudumu na kuwa na faida iliyokusudiwa.

Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dk. Linda Salekwa ameishukuru serikali kwa ujenzi wa uwanja huo na kueleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kukua kwa uchumi wa mkoa wa Iringa na uchumi wa mwananchi mmojammoja pamoja na kuimarika kwa shughuli za utalii.

Awali akiwasilisha taarifa yake Meneja kwa Kiwanja cha Ndege Iringa, Nduli Ashraph Mohammed amesema kuwa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa kiwanja hicho umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 63.74 ambapo baadhi ya maboresho yaliyofanyika ni pamoja na ujenzi wa njia ya kutua na kurukia ndege yenye urefu wa mita 2100 na upana wa mita 30.

Pia Mohamed amesema kuwa mradi huo umehusisha ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege, barabara ya maungio (Taxiway), maegesho ya ndege, taa za kuongozea ndege pamoja na jengo la muda kwa ajili ya abiria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *