Na Mwandishi Wetu,Kagera
Zao la kahawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa wa Kagera likichangia pakubwa kwenye makusanyo yatokanayo na mazao.
Kwasasa zao hili kinara kwenye Halmashauri ya Bukoba Vijijini lina tishio la ugonjwa wa Bungua mweusi unaoshambulia vibaya zao la kahawa na kuimaliza kabisa.
Tayari kwenye Tarafa ya Katerero, Kata mbili za Kishogo na Kasharu umeingia na kuathiri vibaya baadhi ya mashamba ya wakulima.
Juzi Alhamisi Februari 20, 2025 kwenye Kata ya Kishogo, Kijiji cha Ntoija, Afisa Tarafa ya Katerero Bwanku M Bwanku akiongozana na Maafisa kilimo wa Kata ya Kishogo Emiliana Emmanuel na Naomi Myavu, Mtendaji wa Kata (WEO) Mwombeki Balakaijuka na wakulima wametembelea kwenye mashamba ya kahawa yaliyoathirika kuona ugonjwa huu ulivyoshambulia mikahawa na kutoa elimu kwa wakulima hao jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huu.

Gavana Bwanku na Wataalamu Maafisa kilimo walifika mashamba ya Mzee Twaraha na kuongoza zoezi la kuwapa elimu wakulima jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huu kwa kuhakikisha wanakata matawi na miche ya kahawa iliyoathirika na kuichoma moto ili kuwateketeza wadudu hao na mazalio yao.
Yote yamefanyika kwa vitendo kwenye mashamba ya kahawa mbele ya wakulima hatua kwa hatua kukabiliana na ugonjwa huu huku wakulima hao wakiaswa kwenda kuelimisha elimu hiyo kwa wananchi wengine ili kutokomeza ugonjwa huu mpya wa Bungua mweusi unaohatarisha zao hili.

Aidha, Gavana Bwanku amezibeba changamoto zote zilizowasilishwa na wakulima hao kuhusu ugonjwa huu na matamanio yao katika kukabiliana nao na kuwaahidi kufikisha changamoto zote kwenye mamlaka.

