Na Mwandishi Wetu,Tabora
WATENDAJI wa vituo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wanaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, leo Aprili 29, 2025 wamekula kiapo na kuweka wazi msimamo wao kwa kutoa tamko la kujitoa uanachama wa vyama vya siasa au kutangaza kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.

Zoezi hilo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora, Isike Mwanakiyungi,watendaji hao pia waliapa kutunza siri za kazi kwa mujibu wa sheria, mbele ya Afisa Mwandikishaji.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maadili na taratibu za Tume, zinazolenga kuhakikisha usimamizi wa uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na bila upendeleo wowote wa kisiasa.


Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuanza Mei 1, 2025 katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora, na litaendelea kwa muda wa siku saba.