Na Mwandishi Wetu,Morogoro
KATIBU Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassani Doyo, ametoa rai kwa taasisi na mashirika kuhakikisha wanazingatia sheria za usajili kabla ya kushiriki katika shughuli za kisiasa, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro katika kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa, Doyo alisisitiza kuwa ni muhimu kwa taasisi hizo kufuata muongozo uliowekwa, kama ilivyo kwa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria, ili kulinda misingi ya demokrasia na kuhakikisha uchaguzi una kuwa huru, haki na amani.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu, huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kutimiza haki yao ya kikatiba.
“Wananchi jitokezeni kutekeleza haki yenu ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa. Haki hii haipatikani kila siku, ikipita fursa ya mwaka huu, itatuchukua miaka mitano mingine kusubiri mageuzi. Acheni kusikiliza wanasiasa wanaopotosha nafasi hii muhimu, tusije kuijutia baadaye,” alisema Doyo.
Kauli ya Doyo, imekuja kipindi hiki cha kuelekea katika maandalizi ya uchaguzi mkuu kote nchini, ambapo wadau mbalimbali wa kisiasa wanahamasisha ushiriki mpana wa wananchi pamoja na kuheshimu taratibu za kisheria za uchaguzi kwa mujibu wa kanuni, hili kukuza demokrasia nchini.