TAWLA ILIVYOPAMBANA KUSAIDIA JAMII KWA MIAKA 35

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

CHAMA Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimesema ndani ya miaka 35 wamefanikiwa kusimamia mambo sita muhimu yakiwemo kuwafikia zaidi ya wananchi milioni saba (7,000,000) kwa kutoa huduma zakisheria.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 20, 2025 katika kuelekea maadhimisho ya miaka 35 ya TAWLA,Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho Tike Mwambipile alisema katika kipindi chote wamekuwa wakitoa msaada wakisheria kwa wanawake na watoto walioko katika mazingira magumu.

Alisema huduma hizo zimekuwa zikijumlisha ushauri wa kisheria, uwakilishi mahakamani, uandaaji wa nyaraka za kimahakama, pamoja na elimu juu ya haki za binadamu na masuala ya kisheria.

“Ili kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto kwa ufanisi
zaidi,TAWLA imefungua ofisi katika mikoa sita nchini,kupitia mtandao huu wa ofisi, TAWLA imeweza kuwafikia zaidi ya wananchi milioni saba (7,000,000) kwa kutoa huduma mbalimbali za msaada wa kisheria,”alisema Mwambipile.

Alisema Ofisi hizo zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza,Dodoma, Tanga, Mbeya na Arusha.

Alisema huduma hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wanawake na watoto kupata haki zao kwa njia ya kisheria, kuimarisha uelewa wa sheria katika jamii, na kupunguza ukatili wa kijinsia.

Alisema TAWLA inaendelea kujikita katika kutoa huduma hizi kwa lengo la kujenga jamii yenye usawa, haki na utu kwa wote.

Alisema jambo lingine ambalo wamefanikiwa kusimamia kukuza usawa wa kijinsia katika Umiliki wa Ardhi-Kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa pamoja na wadau mbalimbali.

Alisema TAWLA imeboresha ushiriki wa wanawake katika utawala wa ardhi, hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema pia amewezesha mafunzo na upitishaji wa sheria ndogo za vijiji zenye mlengo wa kijinsia katika vijiji 178 katika mkoa wa Tanga, Mwanza, Arusha, Pwani, Morogoro,
Kilimanjaro, Njombe na Mbeya lengo la sheria ndogo ni kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kijamii kuhusu ardhi.

“Pia TAWLA imewezesha
takribani wanawake 400 kuweza kupata Hati milki ya kimila pamoja hati milki za ardhi 51 kwa wanawake,”alisema Mwambipile.

Alisema jambo jingine walilofanikiwa kulisimamia katika kipindi cha miaka 35 ni kuhamasisha Sheria na Sera zinazozingatia jinsia.

“Kwa zaidi ya miaka 35, TAWLA imekuwa mstari wa mbele katika kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa, kuhamasisha na kutetea sheria na sera zinazolenga kuleta usawa wa kijinsia
nchini.

“Shughuli hizi zimejumuisha ushiriki wa moja kwa moja katika utungaji wa sheria mpya pamoja na maboresho ya sheria zilizopo ili kuhakikisha kuwa
zinazingatia haki na usawa wa kijinsia,TAWLA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imetoa mchango mkubwa katika mchakato wa maboresho ya sheria na sera kadhaa muhimu,zikiwemo, Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009,”alisema Mwambipile.

Alisema pia TAWLA imekuwa ikitoa ushauri katika marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya
Mirathi na sheria nyingine zinazohusiana na masuala ya urithi, Sheria ya Ndoa ya
mwaka 1971.

“Kupitia kazi hii, TAWLA imeendelea kuimarisha mazingira ya kisheria yanayolinda na kuendeleza haki za wanawake na watoto, na kuchangia katika ujenzi wa jamii yenye usawa na haki kwa wote,”alisema Mwambipile.

Akitaja shughuli nyingine wanazofanya na TAWLA imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake kupitia mafunzo juu ya uongozi, haki za binadamu, na ushiriki katika maamuzi ya kijamii.

Alisema kupitia mafunzo haya, wanawake wengi wameweza kupata uelewa mpana wa haki zao na kujiamini kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo katika jamii
zao.

Alisema kwa ujumla, TAWLA imekuwa chombo muhimu cha kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wanawake na watoto nchini Tanzania, kupitia utetezi wa haki,
elimu ya kisheria, pamoja na ushiriki katika michakato ya kutunga sera na sheria zinazolenga kuimarisha usawa wa kijinsia.

“Katika kipindi cha miaka 35, TAWLA imefanikiwa kuwajengea uwezo wanawake zaidi ya 500 waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi, kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya Taifa.

“Mafanikio haya yanadhihirisha mchango wa TAWLA katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kutoa mchango wa maana katika ujenzi wa taifa lenye usawa na haki kwa wote,”alisema Mwambipile.

Maadhimisho ya miaka 35 ya TAWLA yanafanyika Mei 22 na 23 jijini Dar es Salaam,mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Dk.Dotto Biteko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *