AZAKI KUKUTANA ARUSHA KUJADILI UTAWALA BORA

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

ASASI  za Kiraia (Azaki) zinatarajiwa kukutana kwa siku tano jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya taasisi hizo ambapo miongoni mwa mambo wanayoyatarajia kuyazungumzia ni pamoja na pamoja na Utawala Bora.

 Akizungumza jijini Dar es Salaam Leo Mei 22, 2025  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) Justice Rutenge, alisema maadhimisho hayo yanafanyika Kwa mara ya saba sasa ambapo kwa mwaka huu yataanza Juni mbili mpaka sita jijini Arusha lengo likiwa ni kuyakutanisha mashirika hayo na kujadiliana mambo kadhaa.

“Maadhimisho ya mwaka huu pia katika mijadala yetu  tutaangazia masuala ya utawala bora, uwajibikaji, utoaji wa huduma bora kwa jamii, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na maendeleo jumuishi.

“Pia kutakuwa na mikutano ya kitaalamu, warsha za kujengeana uwezo, kliniki za maarifa na mijadala ya wazi inayowaleta pamoja wadau kutoka nyanja mbalimbali,”alisema Rutenge.

Alisema kwenye maadhimisho hayo pia watathimini mafanikio ya Azaki na kupanga mikakati ya kuimarisha maendeleo ya Taifa kupitia ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.

Alisema kuwa hii ni mara ya saba mfululizo kwa Wiki ya Azaki kufanyika, huku mwaka huu ikiambatana na kaulimbiu isemayo: “Njia gani tunaweza kutumia ili kufikia maendeleo.”

Rutenge alisena kuwa Azaki zimekuwa na mchango mkubwa katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo tayari imekabidhiwa serikalini na inasubiri kuzinduliwa rasmi.

“Azaki zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mawazo, kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kuwa dira hiyo inaakisi matarajio na mahitaji halisi ya Watanzania,” amesema

Awali akizungumzia  maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Nesia Mahenge, alisema lengo ni kukutanisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuwa tukio hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kubadilishana uzoefu na kujadiliana kuhusu namna bora ya kushirikiana katika uendeshaji wa taasisi hizo.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotolewa zinawanufaisha wananchi kwa njia endelevu na shirikishi na kujaduliana kuhusu namna bora ya kushirikiana katika maendeleo endelevu,” amesema Mahenge.

Kwa upande wa Benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kudhamini maadhimisho hayo kwa kuchangia Sh Milioni 40. 

Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Umma na Mashirika Binafsi, Doreen Dominic, alisema udhamini huo unaakisi dhamira ya benki hiyo katika kusaidia maendeleo shirikishi.

“Huu ni mwaka wa nne mfululizo tunashirikiana na Azaki, na tunaamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na mazungumzo ya wazi, ushirikiano na kuaminiana,” alisema Dominic.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Bora Initiative, Ismail Biro, amesema wiki hiyo itaangazia pia changamoto zinazozikumba Azaki na njia bora za kuzitatua kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, huku makundi maalum kama vijana, wanawake na watu wenye ulemavu yakipewa kipaumbele.

FCS imehimiza washiriki kujisajili mapema ili kuhakikisha wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wote wenye nia ya dhati ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *