Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imetoa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe Leo 22 Mei, hadi tarehe 21 Juni, 2025 kwa Waandishi wa Habari wote wanaofanya kazi za kihabari nchini, kujisajili kupitia Mfumo wa TAI-Habari, ili kuomba kuthibitishwa na kupewa vitambulisho (Press Card).
Taarifa iliyotolewa Leo Mei 22,mwaka 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu WA JAB,Patrick Kipangula imeeleza kuwa waandishi wote wanapaswa kujisajili kupitia kiunganishi cha https://taihabari.jab.go.tz.
” Kabla ya kuingia katika kiunganishi hicho mwombaji anapaswa kuwa na mahitaji yafuatayo, namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) pamoja na ada ya Ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000 kwenye simu kwa urahisi wa kulipa),”amesema Kipangula.

Amefafanua vile vile, mwombaji anatakiwa kuwa na viambatisho vikiwa katika mfumo wa pdf ambavyo ni picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa, vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa na mamlaka husika na kuskaniwa na barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer).
“Mahitaji haya ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa urahisi,”amesema.
Amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 17 (1) (a) ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Tangazo la Serikali Na. 18 la tarehe 03 Februari, 2017 wanaopaswa kujisajili na kupewa Ithibati ni pamoja na Waandishi wa habari, Wahariri, Waandishi wa kujitegemea (Freelancers na Correspondents), Watangazaji wa Radio na Televisheni, Wapiga picha, Waandaaji wa vipindi vya habari (News Producers) na Waandishi wa habari wa kigeni.
Amesema kutokana na uwepo wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu, waandishi wote wa habari watakaotekeleza majukumu ya kihabari yanayohusiana moja kwa moja na mchakato wa uchaguzi huo wanapaswa kuwa wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
“Bodi inawahimiza Waandishi wa Habari kutumia ipasavyo muda uliotolewa kwa ajili ya kujisajili na kupata vitambulisho, ili waweze kufanya kazi za kihabari kwa mujibu wa sheria. Usajili huo pia utatoa fursa ya kuundwa kwa Baraza Huru la Habari, kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 24 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura 229,”amesema,