Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imetengeneza faida ya Sh Bilioni 44 kabla ya kodi katika mwaka wa fedha uliopita huku ikisisitiza kuwa kiasi hicho ni kikubwa zaidi kuwahi kutokea.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Machi 26, 2025 wakati wa mkutano wa 33 wa wanahisa wa benki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Adam Mihayo,alisema pamoja na mwaka jana kupata hasara lakini mwaka huu wa fedha wamepata mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la faida kwa kiasi kikubwa.

“Benki imetengeneza faida ya Sh Bilioni 44 kabla ya kodi,pia mapato yasiyo na riba yameongezeka,benki pia imeweza kuokoa asilimia kumi ya fedha iliyopangwa kutumika,”alisema Mihayo.
Alisema katika mwaka uliopita mali za shirika zimekua kwa asilimia 25 ambapo zimekuwa kwa kasi ukilinganisha na ukuaji wa mali zakibenki.

Alisema ndani ya mwaka huu mikopo imetoka kwa asilimia ishirini huku ukwasi umekua asilimia 16.
“Ongezeko hili kwa mwaka huu imeonesha watanzania na wateja kwa ujumla wameonesha uaminifu mkubwa katika benki hii,”alisema Mihayo.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya TCB Martin Kilimba alisema ni mkutano huo ni fursa ya kipekee kwa wanahisa kutafakari kuhusu utendaji wa benki hiyo, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na kupanga mikakati ya benki yetu kwa siku zijazo.
“Utendaji wa benki yetu mwaka jana unaakisi dhamira yetu ya wazi katika kupanga mikakati inayolenga ukuaji, ubunifu, na katika kukidhi mahitaji ya mteja.

“Vilevile, uwekezaji wa kimkakati katika teknolojia ya kidijitali unaelezea dhamira yetu ya kuboresha ufanis katik utendaji wetu wa kazi,”alisema Kilimba.
Alisema mbali na kurahisisha utendaji wa kazi, hatua hii pia inajenga taswira kwamba sisi nì taasisi inayoendana na mabadiliko yaliyopo katika sekta ya fedha nchini na duniani kwa ujumla.

Alisema kama benki wanasukumwa na dhamira yao ya kuboresha ufanisi wetu na kujitahidi kumridhisha mteja.
“Tumedhamiria kusikiliza na kuelewa mahitaji ya wateja wetu tukijua wazi kwamba imani yao kubwa kwetu inaimarika siku hadi siku. kujizatiti kuwapa suluhisho la mahitaji mbalimbali ya kifedha katika kuchangia mafanikio ya Watanzania,”alisema Kilimba.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, wanakusudia kuendelea kuboresha ufanisi ili kuwezesha ukuaji wa taasisi hii.
“Malengo yetu ni kuendelea kuboresha mizania, kujenga taswira mpya ya taasisi yetu, kutumia fursa zinazoletwa na teknolojia ya kidijitali, kufanya uhakiki wa hasara, pamoja na kusimamia rasilimali watu.

“Tunaamini mambo haya yatatupeleka katika kilele cha mafanikio na kuongeza thamani kwa wanahisa wetu,”alisema Kilimba