Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa,halmashauri za mitaa kuona umuhimu wakulinda Taifa pamoja na rasilimali zilizopo nchini ikiwemo za nishati ya umeme ili kuendelea kutunza usalama wa nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Juni 24, 2025 katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa,Halmashauri za Manispaa Kinondoni na Ubungo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) alisema ni muhimu viongozi hao kupewa semina mara kwa mara ili kuweza kujua nafasi zao katika usalama wa nchi na mali zake kwa ujumla.
Alisema miundombinu ya umeme imekuwa ikiharibiwa huku viongozi wa serikali za mitaa wakiwa wanafahamu.

“Umeme ni ajira,umeme ni maisha kuna watu wanapumulia machine kupitia oksijeni,kulikuwa na tatizo kubwa lakuiba na mafuta ya transfoma na wizi ulikuwa unafanyika wakati watendaji wa mkoa wapo na watendaji wa serikali za mitaa wapo,”alisema Chalamila.
Alisema Tanesco wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha wizi wa mafuta na transfoma unaisha hivyo wenyeviti wanapatiwa semina kwakuwa wao ndiyo walinzi wa malighafi ya Taifa.

“Mnatakiwa kupewa semina ili muweze kufahamu umuhimu wakulilinda Taifa lenu,tunapozungumzia umuhimu wakulinda Taifa ni kitu cha muhimu mitaa mingi wenyeviti wanazungumzia madili na sio usalama.
“Mtu anaona usalama kama ni jukumu la watu fulani,unaweza unaona unakaa leo unakula unashiba lakini kesho Taifa linaingia kwenye matatizo,unaingia kwenye matatizo bila mwenyewe kujijua,”alisema Chalamila.
Alisema kwenye mitaa kunaweza kukatokea mtu mmoja au wawili wakapata hitilafu mpaka wakafariki ama kwakuchoma visu huwezi kusema Tanzania si nchi ya Amani kwakuwa ukifanya tafiti sahihi kuna nchi kila siku inaokota watu waliofariki.

Alisema wenyeviti wa Serikali za mitaa ni wadau muhimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali kwa kuwa miradi hutekelezwa katika maeneo yao ya kiutawala hata miradi mingi ya TANESCO iko kwenye mitaa hivyo “ni imani yangu kuwa kupitia kikao kazi hiki wenyeviti wote wanakwenda kuwa mabalozi wa kueleza huduma nzuri zinazotolewa na TANESCO pia kulinda miundombinu ya Shirika hilo” Alisema RC Chalamila.
Aidha ameipongeza TANESCO kwa kuona umuhimu wa kukutana na kundi hilo muhimu ili liweze kufahamu kwa kina majukumu ya shirika hilo lakini pia kutoa mawazo na ushauri wa namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za nishati ya umeme kwa wananchi hususani katika mitaa yao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Lazaro Twange shirika limekuwa likifanya kampeni mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanatumia nishati rahisi yakupikia.

“Kwa sasa wataalam wanasema yapo majiko ya umeme ukiyatumia kwa gharama ndogo kuliko nishati yoyote,unaweza kupika chakula kwa uniti moja,”amesema Twange.
Amesema kupitia mkakati huo Tanesco inataka kuhakikisha kufikia 2030 kia mtu anapaswa kuwa anatumia nishati safi.
Amesema Shirika hilo kwa kutambua Wenyeviti wa Serikali za mitaa ni wadau muhimu likaona liandae kikao kazi kwa ajili yao ili kutengeneza mfumo mzuri wa mawasiliano ambao utatusaidia kujua wananchi wanasemaje kuhusu huduma za TANESCO pia wenyeviti wawe na uwezo wa kuelewa nini kinafanywa na shirika pamoja na kuwaelimisha wananchi walioko katika maeneo yao.

Twange amemkabidhi RC Chalamila na Viongozi wachache wa Mitaa Jiko la Umeme ambalo linatumia umeme kidogo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi kwa Jamii.
