MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA BIASHARA,NGUZO YA HAKI,UKUZAJI UCHUMI WA TAIFA


Na Mwandishi Wetu,Dodoma
 
KATIKA mazingira ya sasa ya kiuchumi yanayoendelea kubadilika kwa kasi, upatikanaji wa haki kwa haraka, haki na usawa ni msingi muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.
 
Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia Divisheni ya Biashara, imekuwa chombo mahsusi kilichoanzishwa kwa lengo la kutoa majibu ya haraka na yenye tija katika migogoro ya kibiashara, ambayo mara nyingi hujumuisha fedha nyingi na wahusika wakuu katika mnyororo wa uzalishaji wa uchumi.
 
Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ilianza rasmi kazi zake mwaka 1999, ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyokuwa yakiendelea ndani na nje ya nchi ambapo  Serikali iliona ni muhimu kuwa na chombo maalum cha kushughulikia migogoro ya kibiashara kwa ufanisi ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuhakikisha mzunguko wa fedha hauzuiliwi kwa muda mrefu kutokana na mashauri yanayosubiri kusikilizwa kwa miaka mingi.


 
Kuanzishwa kwa mahakama hii maalum kulikuwa ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha kuwa fedha zilizokwama kwenye migogoro zinarejea haraka katika mzunguko wa kiuchumi, kusaidia ukuaji wa sekta binafsi, na kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika mfumo wa utoaji haki nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Msaidizi wa Jaji wa Sheria kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Kelvin Ndomba, Mahakama hii hujihusisha na usikilizaji wa mashauri ya madai yenye asili au sura ya kibiashara.
Miongoni mwa mashauri yanayosikilizwa ni yale yanayohusu mikataba ya kibiashara kama vile mikopo baina ya benki na watu binafsi au makampuni, mikataba ya bima, na migogoro ya kampuni chini ya Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002.
 
Ndomba anasema kuwa Mahakama pia hushughulikia migogoro inayohusiana na hisa, usimamizi na ufilisi wa kampuni, pamoja na usajili na utekelezaji wa tuzo mbalimbali za kibiashara ambazo mara nyingi hutokana na usuluhishi wa migogoro na Mahakama hutumika kuzitambua kisheria ili zitekelezwe kwa nguvu ya kisheria kama hukumu ya Mahakama.
 
Utaratibu wa kufungua na usikilizwaji wa mashauri
 
Mtu anayehitaji kufungua shauri katika Mahakama hii hufuata utaratibu wa kawaida kwa kuwasilisha hati ya madai.
 
Hata hivyo anasema, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ina kanuni zake maalum zilizoanzishwa mwaka 2012 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019, ambazo huongoza mchakato mzima wa usikilizaji wa mashauri hayo.
 
Anasema baada ya kufunguliwa kwa shauri, pande husika hutakiwa kuwasilisha majibu yao kwa maandishi. Hatua inayofuata ni usuluhishi, ambapo msuluhishi husaidia pande mbili kuafikiana kwa hiari bila kutoa hukumu. Iwapo suluhu haipatikani, shauri hurudishwa mbele ya Jaji kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.


Ushahidi wa Maandishi na Mchakato wa Kesi
 
Tofauti na mashauri ya kawaida yanayohitaji mashahidi kutoa ushahidi mahakamani kwa mdomo, Mahakama ya Biashara huhusisha ushahidi wa maandishi. Shahidi huwasilisha ushahidi wake kwa maandishi kabla ya usikilizwaji, na wakati wa kesi, huja tu kuomba Mahakama ipokee ushahidi huo kama sehemu ya maelezo yake hatua ambayo hupunguza muda wa usikilizwaji wa mashauri kwa kiasi kikubwa.
 
Baada ya ushahidi kuwasilishwa, mawakili wa pande husika hufanya maswali ya kinzani na hatua ya mwisho ni kufunga shauri na Mahakama hutoa hukumu baada ya kupitia hoja na vielelezo vyote.
 
Usuluhishi Kama Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro
 
Ndomba anaeleza kuwa usuluhishi ni miongoni mwa mbinu muhimu ya utatuzi wa migogoro inayotumika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.
 
Msuluhishi husaidia pande mbili zenye mgogoro kufikia makubaliano bila ya kutoa hukumu. Matokeo ya usuluhishi ni tuzo maalum inayowasilishwa mahakamani ili kutambuliwa kisheria huku akisema faida ya usuluhishi ni kuwa unaharakisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na kwa gharama nafuu.
 
Faida za Mahakama ya Biashara kwa Uchumi wa Taifa
 
Akielezea faida za uwepo Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara anasema,ina mchango mkubwa katika kuimarisha mzunguko wa uchumi kwani mashauri mengi yanayowasilishwa mahakamani hapo yanahusisha fedha nyingi.
 
“Mashauri yanaletwa katika mahakama hii huwa yanahusisha fedha nyingi ,ni trilioni za fedha ,kwa hiyo uamuzi wa haraka unasaidia kuondoa vizuizi vya kiuchumi kwa kuruhusu fedha hizo kurudi katika mzunguko na kusaidia wawekezaji kuendelea na shughuli zao za uzalishaji.
 
Mahakama hii pia ina muda wa juu uliowekwa kisheria wa miezi 10 wa kumaliza mashauri tangu kufunguliwa kwake, jambo linalopunguza ucheleweshaji wa haki na kuwavutia wawekezaji kwa kuwa na uhakika wa mazingira rafiki ya kibiashara.
 
Licha ya mafanikio ,Ndomba anaeleza na changamoto zilizopo katika mashauri hayo ambapo anasema ni pamoja na baadhi ya makubaliano ya usuluhishi hushindwa kutekelezwa kikamilifu hasa pale ambapo wahusika hushindwa kutimiza masharti ya kifedha waliyojiwekea.
 
“Kwa mfano kushindwa kulipa kwa mikupuo kama walivyokubaliana maana hili jambo linahusisha fedha,kwa hiyo wakati mwingine mtu anaweza kukwama.”anasema Ndomba
 
Hata hivyo, Ndomba anasisitiza kuwa idadi kubwa ya mashauri yanayopitia usuluhishi huishia kwa mafanikio.
 
Elimu kwa Umma
 
Ndomba anasema,ili kujenga uelewa kwa umma kuhusu shughuli za Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ,wamekuwa wakitoa elimu kwa kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari pamoja na maonyesho mbalimbali yakiwemo ya Kimataifa ya Biahsra maarufu kama Sabasaba.
 
Anasema katika Maonyesho ya  Sabasaba mwaka huu 2025 ,pia wamefanya shughuli hiyo ya kelimisha umma kwa wananchi waliofika kwenye banda lao
 
“Katika maonyesho ya Sabasaba, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imekuwa ikishiriki kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zake. Lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi, hasa wafanyabiashara na wawekezaji, wanatambua kuwa wana sehemu salama ya kupeleka mashauri yao ya kibiashara na kutatuliwa kwa wakati.”anasisitiza Ndomba
 
Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ni mhimili muhimu wa mfumo wa haki nchini Tanzania. Kwa kutoa haki kwa haraka, kurahisisha mzunguko wa fedha na kusaidia wawekezaji kupata suluhu ya migogoro yao kwa ufanisi, Mahakama hii inabeba jukumu kubwa katika kuimarisha uchumi wa taifa.
 
Ni wajibu wa kila mwananchi, hasa wadau wa biashara, kuelewa uwepo na majukumu ya Mahakama hii na kuitumia ipasavyo kwa manufaa ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.