UWEKEZAJI WA DK.SAMIA KWENYE MIUNDOMBINU WAIPA UWEZO NA UBORA TMA KUTABIRI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Dk. Ladislaus Chang’a ameeleza kuwa ubora wa taarifa zao umeendelea kuongezeka na kuimarika kwa sababu ya uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya uangazi na ya utoaji wa taarifa ya hali ya hewa.

Pia sababu nyingine ni uwekezaji katika kuimarisha rasilimali watu ambapo takribani wafanyakazi 97 wa TMA wapo sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa masomo ya kuongeza umahiri na weledi.

Hayo ameyasema Agosti 3,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la mamlaka hiyo kwenye maonesho ya wakulima na Wafugaji kitaifa ambayo yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini hapa,alisema kwa sababu hizo TMA wanaendelea kufanya vizuri na kupewa nafasi ya kuweza kuzisaidia nchi nyingine ndani ya Bara la Afrika huku akisema hivi karibuni wataalam wao walienda nchi za Burundi,Sudani ya Kusini.

“Mwaka jana tulienda Namibia lakini pia wenzetu wa Zimbabwe walikuja kujifunza kwetu na wenzetu wa Uganda wanatarajia kuja kujifunza kwetu pia tuna maombi ya wenzetu kutoka nchi za Guinea, Sierra Leone, Gambia na wanatamani tuweze kuwasaidia katika baadhi ya maeneo,” alisema.

Aliongeza kuwa yote hayo yanatokana na uwekezaji wa serikali ya Dk. Samia katika kuimarisha miundombinu pamoja na rasilimali watu.

Alisema kama kaulimbiu ya maonesho hayo inavyosema ‘Changua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’ hivyo wanatumia fursa hiyo kuendeleza kusisitiza hilo huko akisema nao wanasema tumia taarifa za hali ya hewa kuweza kuleta tija katika kilimo na shughuli zote za kiuchumi kadri inavyowezekana.

“Mamalaka ya hali ya hewa tupo nane nane hapa Dodoma vile vile tupo Zanzibar, Morogoro na Mbeya kwa muktadha mzima wa kuangalia namna ya kuitumia fursa hii katika kuendeIea kuelimisha jamii ya kuhamasisha matumizi sahihi ya taarifa ya hali ya hewa katika kuongeza ufanisi na tija kwenye shughuli za kilimo, kijamii na kiuchumi kwa ujumla wake,” alisema.

Alisema kuwa hayo yote yanapata msukumo zaidi kutokana na na changamoto kubwa ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo dunia nzima wanashuhudia hali hiyo inazidi kubadilika, joto linadizi kuongezeka.

Alifafanua miezi mitatu iliyopita waliendelea kuzungumza kwamba mwaka 2024 ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye ongezeko la joto zaidi katika historia ya dunia ambapo lilifikia nyuzi joto 1.55 kwa kipimo cha nyuzi joto ambalo halijawaji kutokea tangu walivyoanza historia ya uangazi wa hali ya hewa.

Alieleza kuwa hapa nchini waliona ongezeko la joto lilifikia nyuzi joto 0.7 kiwango ambacho hawajawahi kukipima huku akisema hayo yote yanaambatana na ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.

Alisema wanaendelea kuhimiza wakati na kipindi kama hiki ni muhimu kuzingatia na kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA ikiwamo utabiri w msimu, kila mwezi na wa kila siku pamoja na tahadhari ambazo wanazitoa kila inapobidi.