Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, amepongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, akisisitiza kuwa chuo hicho kina nafasi ya kipekee kama “baba wa vyuo vyote” nchini.
Machali ametoa pongezi hizo leo, Agosti 6, 2025, alipotembelea banda la UDSM katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, amesema amevutiwa na teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na wanafunzi pamoja na watafiti wa chuo hicho, ambazo zinaonyesha namna UDSM inavyowekeza katika ubunifu wa vitendo.

“Tumewaona mabinti wadogo kabisa wakitengeneza bidhaa za thamani kama mafuta ya asili yanayosaidia kuondoa makunyanzi. Hii ni ishara ya mafanikio makubwa ya uwekezaji wa UDSM katika ubunifu unaogusa maisha ya watu moja kwa moja,” amesema Mhe. Machali.
Aidha, ameeleza kufurahishwa na teknolojia ya kisasa katika sekta ya ufugaji wa samaki, hususan mashine ya kukamata vifaranga bila kutumia mikono, ambayo inapunguza vifo vya vifaranga kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na njia za kawaida.

“Kwa mujibu wa wataalamu, kutumia mikono kunahatarisha maisha ya vifaranga kwa zaidi ya asilimia 25, lakini kwa kutumia mashine hii ni nadra sana vifaranga kufa,” amebainisha.
Kutokana na hilo, Machali amewataka wazalishaji wa vifaranga na wafugaji nchini kwa ujumla kutembelea banda la UDSM ili kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hizo, akisisitiza kuwa zitawasaidia kuboresha uzalishaji na kupunguza hasara.

Katika hatua nyingine, amesifu maendeleo ya kidijitali yanayoendelezwa na UDSM kupitia programu za simu (apps) zinazowaunganisha wakulima moja kwa moja na watoa huduma za kilimo, jambo alilolieleza kuwa linapunguza hitaji la wakulima kusafiri kwenda kwa maafisa kilimo.
“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu. Kupitia apps hizi, mkulima anaweza kupata huduma zote za kilimo akiwa kijijini kwake bila kuhangaika,” amesema.

Akihitimisha, Machali ameipongeza UDSM kupitia Ndaki ya Masuala ya Kilimo na Teknolojia zake kwa jitihada kubwa na mchango wa moja kwa moja kwa maendeleo ya Taifa.
