MBUNGE KIBAHA ADAIWA KUHARIBU MCHAKATO KURA ZA MAONI

Na Mwandishi Wetu,Pwani

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  katika jimbo la Kibaha Mjini wilayani ya Kibaha mkoani Pwani wamedai kuwa uchaguzi wa ndani wa chama hicho ulitawaliwa na  vitendo vya rushwa na kusababisha wajumbe kupitisha viongozi wasiokuwa waadilifu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi na wananchi wa eneo hilo walidai kuwa kuna haja ya kubadilisha utaratibu wakuchagua viongozi hao kutoka kutumia wajumbe badala yake watumie  wanachama wa kawaida kwakuwa kundi linalochagu viongozi ni watu wachache na rahisi kupewa rushwa.

Mmoja wa wanachama hao ambaye ni diwani mstaafu wa kata ya Msangani Genze Chongela alisema katika  uchaguzi huo hatua za awali  zilienda kwa haki lakini wakati wa kupiga  kura hakukuwa na  haki kwa sababu rushwa zilitembea sana kwa wajumbe.

“Hawa wajumbe wa nyumba kumi tunaowatumia ni rahisi sana kupewa rushwa ilifika mahali watu wanapewa hadi laki laki za rushwa kwa muda mmoja.

“Hakuwezi kuwa na uchaguzi bao mbunge alishasema ametenga Sh Milioni 200 kwa ajili yakuangusha madiwani ambao hawapo upande wake,kila ambaye alikuwa hatetei maslahi yake jimbo alikatwa,”alisema Chongela. 

Alisema huku akitolea mfano kwake ambapo anadai uadui ulianza  baada ya yeye yakumuoa adui yake.

“Alishasema ataweka Sh Milioni 200 kuning’oa kisa nilioa mtu ambaye adui yake  na nimeangushwa na kweli,aliapa madiwani wote waliopinga shughuli zake zakimaslahi wataondoka na amehakikisha wote kumi hatujachaguliwa,”alisema Chongela.

Naye Mjumbe wa shina namba nane  Ramdhani Ngoda  alisema hajaridhishwa na mchakato huo 

kwakuwa  rushwa ilitumika kwa kiasi kikubwa kufadhili watu waangushwe.

“Sisi kilio chetu tunakipeleka kamati kuu kutokanana uchafu huu wanapaswa kuangalia  mtu sahihi kuanzia kwenye ubunge hadi madiwani ili waweze kumrudisha kwa wananchi ili apeperushe bendera ya chama,”alisema Ngoda.

Alisema  hajaridhishwa na uchaguzi huo mpaka sasa hajui mbunge na madiwani wameshindaje.

“Nimepiga kura lakini katika kupiga  kura sikufurahishwa  kwakuwa kiongozi tuliyokuwa tunamtaka na viongozi wengi wanamtaka alishindwa na akapata yule yule ambaye amekaa  miaka 15  kwa kweli mimi sikufurahishwa kwa sababu kweli mtu tunakuchagua miaka 15 shida yetu dhiki yetu hujui.

“Sisi tuna mikutano tisa,mikutano mitatu  tunafanya kila baada ya miezi  mitatu,mkutano unamtaka  diwani na mbunge awepo pamoja na  wanachama  unatakiwa uje utoe maoni lakini mbunge hatumuoni lakini kaja kipindi cha uchaguzi tu na kashinda,tunajiuliza kashindaje,”alisema Ngoda.